Wanafunzi saba shule ya Ghati Memorial wahofiwa kufa maji Arusha

Muktasari:

  • Wanafunzi saba wa Shule ya Msingi Ghati Memorial wanahofiwa kufariki dunia baada ya gari la shule waliokuwemo kuangukia kwenye korongo lililojaa maji eneo la Dampo kata ya Muriet mkoani Arusha.

Arusha. Wanafunzi saba wa Shule ya Msingi Ghati Memorial wahofiwa kufariki dunia baada ya gari la shule waliokuwemo kuangukia kwenye korongo lililojaa maji eneo la Dampo, Kata ya Muriet mkoani Arusha.

Korongo hilo lililojaa maji yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku usiku wa kuamkia leo April 12, 2024, ilisababisha maji kujaa hadi  barabarani.

Wakizungumza katika eneo la tukio, mashuhuda wamesema kuwa saa 12 asubuhi, gari lenye namba  za usajili T 496 EFK  lilikatiza juu ya barabara hiyo, dereva alishindwa kulidhibiti, hivyo liliyumba kabla ya kuangukia katika korongo hilo linalomwaga maji yake katika mto mkubwa wa Themi.

 Lilian Mussa, amesema baada ya watu kuona hali hiyo walisogea eneo la tukio na kufanikiwa kuokoa watoto wanne kabla ya gari kuendelea kusogea tena na watoto wengine walionekana kusombwa na maji.

“Dereva alipoona gari linamshinda aliruka ndio watu wakaona wakaanza kusaidia hao watoto, lakini gari lilizidi kusogea kwenye kina tukaamua kuita Jeshi la Zimamoto na Polisi,” amesema Lilian.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto Mkoa wa Arusha, Osward Mawanjejele amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema kwa taarifa za awali ni kwamba gari hilo lilikuwa na watoto 11 na walimu wawili.

“Niko kwenye msafara wa Rais kwa ajili ya tukio la maadhimisho ya miaka 40 ya kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine, lakini kikosi hadi sasa wananiambia wameokoa watoto wanne na walimu wawili… bado wanaendelea kufuatilia wengine wanaosemekana walikuwepo kwenye hilo gari,” amesema.

Amesema kikosi chake kimeelekeza nguvu katika mto Themi ambapo korongo hilo linamwaga maji yake, ili kuona namna ya kuwaokoa watoto wengine wanaodaiwa walikuwepo ndani ya gari hilo.