Wanafunzi Songea wafundwa utunzaji mazingira

Muktasari:

Wanafunzi wa shule ya Msingi, Litowa Wilaya ya Songea wametakiwa kuwa mabalozi wa mazingira kwenye maeneo yao na kuwaelekeza wazazi wao athari zinazotokana na shughuli zinazochangia  uchomaji ovyo moto misitu kwa ajili ya kuandaa mashamba, mkaa, kilimo cha kuhama hama na ufugaji wa mifugo mingi.

Songea. Wanafunzi wa shule ya Msingi, Litowa Wilaya ya Songea wametakiwa kuwa mabalozi wa mazingira kwenye maeneo yao na kuwaelekeza wazazi wao athari zinazotokana na shughuli zinazochangia  uchomaji ovyo moto misitu kwa ajili ya kuandaa mashamba, mkaa, kilimo cha kuhama hama na ufugaji wa mifugo mingi.

Wito huo umetolewa na Mratibu wa programu ya kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao ya msitu ( FORVAC) Mkoa wa Ruvuma, Marcel Mutunda wakati wa kongamano  kuhusu umuhimu wa Misitu na mabadiliko ya tabia nchi kwa wanafunzi wa shule ya Msingi Litowa Kijiji Cha Litowa.

Amesema  alimu zaidi ya Utunzaji Mazingira inahitajika kwa watoto wadogo ili waweze kueneza Elimu hiyo kwa wazazi wao na jamii kwa ujumla ndio maana wameona wawapatie elimu ya Utunzaji Mazingira watoto hao kwa vitendo ili hata wanapokuwa wawe wakifahamu umuhimu wa Utunzaji wa Misitu na faida zake.

"Kumekuwa na uharibufu mkubwa wa Misitu kwa kufanya shuguli za kilimo,ukataji kuni kwa ajili ya kuchoma mkaa, ukataji miti ovyo kwa ajili ya nishati ya kupikia, ufugaji mifugo mingi kwenye eneo dogo hali ambayo inasababisha kukosekana kwa mvua za uhakika,na uharibufu wa vyanzo vya maji hivyo kuleta athari kwa jamii ikiwemo mabadiliko ya tabia ya nchi,"amesema Mutunda

Aidha pamoja na mafunzo hayo wanafunzi wamepatiwa miti na kufundishwa kuipanda kwa ajili ya kuwaletea kivuli na mbao ili kuzuia uharibufu wa Mazingira ambapo wataitunza na wameweka vibao vya majina Yao.

Naye Ofisa Misitu halmashauri ya Wilaya ya Songea, Zakayo Kaunda amewasisitiza wanafunzi hao kuhakikisha wanaitunza vema miti hiyo ikiwa ni pamoja na kupanda miti kwenye Mazingira wanayoishi.

Kwa upande wake kaimu Ofisa Elimu Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Sixberth Komba amemshukuru kwa kuweza kutoa Elimu kwa vijana hao kwani itawasaidia kuendelea kuhifadhi Mazingira endelevu kwa vizazi vilivyopo na vijavyo.

Naye mwanafunzi Isaya soko amesema Elimu waliyopata itawasaidia kwenda kuanzisha bustani ya miti ya matunda na mbao ambapo pamoja na kutunza Mazingira pia wataweza kupata matunda na kufuga nyuki hivyo kupata asali na nta watatengenezea mishumaa ambayo watauza na kupata mahitaji ya shule pamoja na ada.