Wanafunzi waliorudishwa Ukraine waingizwe vyuoni
Mbunge wa Viti Maalumu, Jane Jerry Ntate
Muktasari:
- Serikali imeombwa kuwasaidia wanafunzi wa Kitanzania waliorudishwa nchini kutokana na vita ya Ukraine na Urusi.
Dodoma. Mbunge wa Viti Maalumu, Jane Jerry Ntate ameiomba Serikali kuwarejesha kwenye vyuo vya Tanzania wanafunzi waliorejeshwa nchini kutokana na vita vya Ukraine na Urusi.
Ntate amesema hayo leo Jumanne Juni 20, 2023 wakati akichangia bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2023/2024 katika Bunge la 12 mkutano wa 11 kikao cha 51.
“Lakini nishukuru kilichofanyika jana tumeona kwenye mitandao, tumeruhusu wanafunzi wa Sudan kuja kumalizia masomo Tanzania.” amesema na kuongeza kuwa;
“Niiombe Serikali kuna watoto wetu ambao walirudi kwa ajili ya vita kutoka Ukraine, m paka sasa hivi hatujafanya utaratibu warudi kwenye vyuo.”
Kwa upande mwingine Mbunge huyo amehoji: “Lakini, leo tumeleta hawa nje, hivi hawa wa hapa wanajisikiaje, ni madaktari ambao wanweza kusaidia nchi, wengine ni wahandisi, zingine ni taaluma mbalimbali, basi nao warudishwe kwenye vyuo wakaendelee na masomo,” amesema.
Wanafunzi wa Sudani
Jana Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Profesa Mohamed Janabi alitangaza kuwahamishia wanafunzi 150 wa udaktari kutoka Chuo Kikuu cha Tiba, Sayansi na Teknolojia (UMST) cha Khartoum nchini Sudan.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, wanafunzi hao wamehamishiwa MNH ili kukamilisha masomo yao kufuatia mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yanayoendelea nchini humo.
Warejeshwa nchini
Machi mwaka jana kundi la Wanafunzi tisa kati ya 11 waliokuwa wamekwama Summy nchini Ukraine na baadaye kufanikiwa kuvuka mpaka na kuingia Urusi, walirejeshwa nyumbani nchini Tanzania na kupokewa kwa furaha na ndugu na jamaa.
Urusi ilitengeneza njia ya usalama kuwawezesha wanafunzi wa Tanzania waliokuwa katika Chuo Kikuu cha Sumy (Sumy State University) ili kuepuka mashambulizi ya vita vinavyoendelea nchini Ukraine.
Vita vya Sudani
Misukosuko imetawala kipindi cha mpito kuelekea utawala wa kiraia nchini Sudani, tangu Rais wa zamani wa taifa hilo Omar Hassan El-Bashir apinduliwe Aprili, 2019.
Serikali ya mpito ya kiraia iliyowekwa madarakani baadaye mwaka huo, kupitia makubaliano ya kugawana madaraka kati ya viongozi wa kijeshi na wa kiraia, ilipinduliwa kupitia mapinduzi ya kijeshi Oktoba, 2021. Tangu wakati huo, taifa hilo halijawa na serikali inayoongozwa na raia.
Matumaini ya utawala wa kiraia yaliota mbawa baada ya mapigano kuibuka Aprili 15, kati ya Jeshi la Serikali, (SAF), likiongozwa na Luteni Jenerali Abdel-Fattah Al-Burhan, na wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF), wakiongozwa na Luteni Jenerali Mohamed Hamdan Dagalo, wakiacha mamia ya watu wamekufa na maelfu kukimbia nchi.