Wanafunzi wanaoacha shule tishio jipya Tanzania

Muktasari:

  • Takwimu  zinaonesha katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuna ongezeko la zaidi ya mara mbili la watoto wanaoacha shule kwa shule za msingi.

Dar es Salaam. Baada ya juhudi za Serikali kuhakikisha watoto wanakwenda shule kwa kusimamia sera ya elimu bure, mkazo zaidi unahitajika kuhakikisha watoto hao wanabaki shuleni kupata elimu.

Hiyo inatokana na takwimu msingi zinazotolewa na Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kuonyesha ongezeko la watoto wanaoacha shule kwa sababu mbalimbali.

Takwimu hizo zinaonesha katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuna ongezeko la zaidi ya mara mbili la watoto wanaoacha shule kwa shule za msingi.

Jumla ya watoto 167,834 waliacha shule katika shule mbalimbali za msingi nchini kwa mwaka 2019 ukilinganisha na watoto 66,142 walioacha shule mwaka 2017.

Taarifa hiyo inabainisha ongezeko la zaidi ya mara mbili ya uwiano wa wanafunzi walioacha shule kwenye walioandikishwa shule za msingi. Ongezeko hilo ni kutoka asilimia 0.7 hadi asilimia 1.6 katika kipindi hicho.

Samwel Moroga, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kiyange katika Halmashauri ya Buhingwe mkoani Kigoma, anasema uelewa wa mzazi juu ya umuhimu wa elimu una mchango mkubwa sana kwenye maendeleo ya mtoto.

“Mtoto atakuwa na makundi rika na hataulizwa kwa sababu mzazi hajui umuhimu wa elimu. Watoto wengine pia hutoroka shuleni kwa kuogopa adhabu wanazopewa na walimu,” alisema.

Dk Jimso Sanga, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Iringa anasema utoro kwa wanafunzi unatakiwa uangaliwe kwenye maeneo yenye vishawishi kama kuna mazingira ya ajira kwa watoto, kuingizwa katika ufugaji, kutunza familia kisha kuyatafutia ufumbuzi.

Takwimu zinaendelea kuonesha kuwa watoto wa kiume wanaoacha shule wameongezeka hadi asilimia 58 ya watoto wote ukilinganisha na asilimia 55 kati ya mwaka 2017 na 2019. Hii ina maana kuwa jumla ya watoto 96,683 wa kiume waliacha shule mwaka 2020 ukilinganisha na watoto wa kike 71,151. Mwaka 2017 ilikuwa wavulana 36,434 na wasichana 29,708.

Kupitia takwimu hizo, utoro wa rejareja ulichangia asilimia 94 ya wanafunzi kuacha shule mwaka 2017 na asilimia 97.5 mwaka 2019.

Hii ina maana wanafunzi 167,834 waliacha shule kutokana na utoro wa rejareja mwaka 2020, huku sababu nyingine zilizotajwa ni mimba, vifo na nidhamu.

Sababu hizo zilichangia wanafunzi kuacha masomo kwa asilimia 0.7, asilimia 1.8 na asilimia 0.1 katika mtiririko wa awali.

Kati ya wanafunzi walioacha shule kwa utoro, makundi mabaya yalichangia kwa asilimia 17.8, ukosefu wa mahitaji muhimu kwa asilimia 14.5, jambo ambalo limewaathiri wavulana kuliko wasichana na nyingine ni asilimia 45.8.

Mbali na sababu hizo, nyingine zilizotajwa ni ufugaji, biashara ndogondogo, kukosa mahitaji muhimu, kupeana talaka wazazi, kuwaangalia wazazi na ndugu zimechangia sana wanafunzi kuacha masomo.

Wakati utoro ukisalia kuwa sababu kuu kwa miaka mitatu mfululizo, mwaka 2019 mkoa wa Simiyu uliongoza baada ya wanafunzi 19,496 ambao ni sawa na asilimia 4.1 ya waliodahiliwa kuacha shule.

Kati ya wanafunzi hao, wavulana ni 11,141 na wasichana ni 8,355. Licha ya kuwa ni asilimia 3.5 ya wanafunzi waliacha shule mkoani Geita, kwa idadi ya wanafunzi ni 21,969, ambao ni wengi kuliko wa mikoa yote.

Mikoa mingine

Baada ya Simiyu na Geita, Kagera inafuata ikiwa na wanafunzi 17,274 walioacha shule, Tabora 15,566 na Mwanza 13,845.

Ni wanafunzi 520 pekee ndio waliocha masomo mwaka 2019 mkoa wa Dar es Salaam, idadi ambayo ni sawa na asilimia 0.1 ya udahili ikiwa ni wanafunzi wachache zaidi.

Darasa linaloongoza

Takribani nusu ya wanafunzi wote walioacha chule walikuwa darasa la tatu na nne. Katika mwaka huo, wanafunzi 52,684 wa darasa la nne waliacha masomo, huku 42,765 wakiwa wa darasa la tatu kwa mwaka 2019.

Hii ni tofauti na mwaka 2017 ambapo darasa la kwanza na la pili ndio waliokuwa wanaongoza kwa kuacha shule kwa asilimia 41.


Wadau wafunguka

Ofisa Elimu mkoa wa Simiyu, Ernest Hinju anasema katika mikakati wanayoifanya ni kuweka vikao vya wazazi kila mwisho wa muhula wa mwaka ili kuwaeleza umuhimu wa elimu na kuwahimiza watoto wao kuendelea na shule.

Akitaja sababu nyingine alisema “…tunawaasa walimu kuwa walezi wazuri wa wanafunzi wawapo shuleni, mbali na kuwafundisha pia wawaambie nini maana ya kile wanachofanya. Kwa watoto wa kike tumewawekea walezi (matron) ili kupata ushauri na namna gani elimu itawanufaisha”.

Ofisa elimu anasema wanayafanya hayo baada ya kubaini jamii nyingi mkoani humo hawakuona umuhimu wa elimu, “...mtoto akijua kusoma na kuandika basi anaachishwa shule na anaanza kufundishwa umiliki wa ng’ombe, kuangalia mifugo, biashara ndogondogo, kuoa, kuolewa vikionekana ndio muhimu”.

Naye Mwalimu Moroga alisema moja ya njia inayoweza kudhibiti utoro kwa wanafunzi ni kutoa chakula ili kuepusha wao kutoroka wanapohisi njaa, kutengeneza mazingira mazuri ya kujifunzia na walimu kuwa rafiki.

Dk Sanga alieleza kuwa utoro kwa wanafunzi unaweza kumalizika kwa kushughulikia vyanzo vya wao kushindwa kuhudhuria masomo badala ya adhabu pekee.

“Kuwaelimisha wazazi, walezi na watoto wenyewe ili wajue umuhimu wa elimu na baada ya hapo watunga sera waziongezee meno sheria na zitumike, kufanya hivi kutawafanya watu kuogopa kuwafanya watoto wasiende shule na kila wanapotorokea wanakuwa hawapokelewi,” anasema Dk Sanga.

Anasema licha ya kuwa wanaobaki shule ni wengi kuliko wanaoacha, lakini ni vyema kuwa na mkakati wa kuwarudisha wanaoachwa nyuma, waelimishwe, wapewe elimu ya darasani na ustahamilivu shuleni.

“Hiyo ni kwa sababu, kwa wakati huo wanaona wanakotorokea kuna ahueni ya maisha, lakini wanashindwa kutambua kuwa mbele yake kuna kitambo cha majuto,” anasema Dk Sanga.