Wanafunzi waomba sheria wakeketaji kunyongwa hadi kufa
Meneja Rasilimali Watu wa Shirika la Grumeti Fund, Amsi Nyambuche,akizungumza kwenye kongamano la kujadili changamoto zinazowakabili wanafunzi wa kike katika maeneo yanayozunguka mapori ya akiba ya Grumeti na Ikorongo katika wilaya za Bunda na Serengeti pamoja na namna ta kukabiliana na changamoto hizo. Picha na Beldina Nyakeke
Muktasari:
- Adhabu hizo ni pamoja na kutungwa kwa sheria ya kunyongwa hadi kufa wale wote wanaojihusisha na vitendo vya ukeketaji wakiwepo mangariba hatua ambayo wamedai itasaidia kupunguza na hatimaye kumaliza vitendo hivyo katika jamii.
Serengeti. Baadhi ya wanafunzi wa kike kutoka shule za sekondari zinazozunguka mapori ya akiba ya Grumeti na Ikorongo katika wilaya za Serengeti na Bunda, wameiomba Serikali kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii sambamba na kuweka adhabu kali zaidi kwa wanaojihusisha na vitendo vya ukeketaji.
Wamesema adhabu hizo ni pamoja na kutungwa kwa sheria ya kunyongwa hadi kufa, wale wote wanaojihusisha na vitendo vya ukeketaji ambayo wamedai itasaidia kupunguza na hatimaye kumaliza kabisa vitendo hivyo.
Wametoa wito huo leo Jumatatu, Julai 20, 2026 wilayani Serengeti wakati wa kongamano lililoandaliwa kujadili changamoto zinazowakabili wanafunzi wa kike na namna ya kuzitatua.
Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mariwanda, Fatuma Ramadhani amesema elimu kuhusu madhara ya ukeketaji inapaswa kuendelea kutolewa, hasa katika maeneo ya vijijini ambako mila hiyo bado inaendelea kushamiri.
“Ni wakati wa Serikali kuangalia njia mbadala za kumaliza kabisa tatizo hili. Elimu iendelee kutolewa, lakini pia sheria ziwe kali zaidi ili kuwazuia wanaoendelea kufanya ukeketaji,” amesema.
Naye mwanafunzi wa kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Chief Sarota, Abia Ryoba, amesema kuna haja ya kuwa na sheria mahsusi inayobainisha adhabu kwa makosa ya ukeketaji ili kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya vitendo hivyo.
Amesema kwa mtazamo wake, hatua kali dhidi ya wahusika zitasaidia kutoa fundisho kwa wengine na kupunguza matukio yanayoendelea kujitokeza katika jamii.
Kwa upande wake, mwanafunzi Magori Kaitira amesema mtazamo unaodai mwanamke hawezi kuwa kiongozi hauna nafasi katika jamii ya sasa, akibainisha wengi wameonyesha uwezo mkubwa katika ngazi mbalimbali nchini na duniani.
Mwanafunzi Minza Malongo amesema baadhi ya wasichana hulazimika kufanya kazi nyingi za nyumbani baada ya kutoka shuleni, jambo linalowaathiri kitaaluma ikilinganishwa na wenzao.
Kutokana na hali hiyo, wameiomba Serikali na wadau wa maendeleo kujenga mabweni katika shule za sekondari ili kuwawezesha wanafunzi wa kike kusoma katika mazingira salama na yenye utulivu.
Akizungumza katika kongamano hilo, Ofisa Elimu wa Shirika la Grumeti Fund, Elizabeth Magoto amesema wamekuwa wakiandaa makongamano ya aina hiyo kwa zaidi ya miaka 10 ili kuwapa wanafunzi wa kike nafasi ya kujadili changamoto zinazowakabili na kutafuta njia za kuzikabili.
Amesema makongamano hayo yameanza kuzaa matunda, ikiwamo kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa kike wanaoomba ufadhili wa masomo ya elimu ya juu kupitia shirika hilo.
“Kwa sasa tuna uwiano wa karibu asilimia 50 kwa 50 kati ya wavulana na wasichana wanaoomba ufadhili wa masomo. Pia tunaona ongezeko la wasichana wanaochagua masomo ya sayansi, jambo ambalo halikuwa la kawaida hapo awali,” amesema.
Meneja wa Rasilimali Watu wa Grumeti Fund, Amsi Nyambuche, amesema shirika hilo litaendelea kuandaa makongamano hayo kwa lengo la kuwajengea uwezo watoto wa kike kukabiliana na changamoto zinazowazuia kutimiza ndoto zao.