Wanafunzi wawili wafariki kwa kufukiwa na kifusi

Muktasari:
- Kifusi kilichomeguka wakati wakichimba mchanga kilisababisha vifo vya watu wawili.
Dodoma. Wanafunzi wawili wa kidato cha pili katika Shule ya Sekondari ya Mbalawala jijini Dodoma wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa baada ya kufukiwa na kifusi cha mchanga wakati wakichimba mchanga Mbalawala jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CCM wa Kata ya Mbalawala, Athanas Sajilo, waliofariki ni Oscar Richard (19) na Andrea Chibago (19) huku kondakta wa lori la mchanga akijeruhiwa (jina bado halijafahamika).
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Galus Hyera amesema hayo leo Jumanne, Julai Mosi, 2025, akieleza kuwa tukio hilo lilitokea jana Jumatatu majira ya alfajiri.
“Ni kweli tukio hilo limetokea eneo la Mbalawala wakati wakiendelea na shughuli zao za uchimbaji mchanga, kifusi kilimeguka na kuwafukia wananchi wawili ambao ilithibitika kutoka eneo la tukio kwamba wamepoteza maisha,” amesema.
Amesema kuna mmoja aliokolewa na kupelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma ambapo anaendelea na matibabu.
Hyera ametoa wito kwa wanaofanya shughuli hizo kutambua kuwa ni za kiuchumi, huku akiwataka kufahamu kuwa uchumi ni lazima uambatane na usalama.
“Rai yangu ni kwamba pale wanapoona kwamba kazi wanayofanya ni hatarishi, wazingatie zile tahadhari za kuwafanya wamalize kazi zao na kurudi nyumbani wakiwa salama,” amesema.
Pia, amewataka kuzingatia taratibu zinazoelekezwa kuhusu shughuli za uchimbaji madini kutoka Idara ya Madini kwamba uchimbaji ufanyike kukiwa na mwanga wa kutosha.
Amesema kwa kufanya hivyo, dalili za gema kuanguka wanaweza kuzishuhudia na kuchukua hatua haraka za kuepukana na athari hiyo.
Naye Ofisa Uhusiano wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Renatha Mzanje amesema wamepokea miili ya wanaume wawili na majeruhi mmoja ambaye anaendelea na matibabu.
“Majeruhi anaendelea vizuri, hana hali mbaya sana,” amesema bila kutaja majina ya watu hao.
Akizungumza, Sajilo amesema saa 12:00 asubuhi alipigiwa simu na kuelezwa vijana wanaopakia mchanga katika magari walipokuwa wakipakia mchanga katika gari, kifusi kiliporomoka na kuwafukia.
“Kikaporomoka, kikagonga vijana wawili wakafa palepale, wanne walinusurika hawakuwa na majeraha yoyote na kondakta wa lile gari naye kilimpitia akakimbizwa hospitali ya General (Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma),” amesema.
Amesema walipowauliza walionusurika, waliwaeleza kuwa jana waliloweka maji katika machimbo kwa imani kuwa hadi leo watakuta mchanga umeshuka, lakini walipokwenda wakakuta haukushuka.
“Wakawa na imani kuwa bado, sasa kuruhusu ile gari na ule mtikisiko, nahisi ndicho kilichosababisha kishuke kwa haraka (kifusi),” amesema.
Amesema vijana hao wamekuwa wakifanya shughuli hizo wakati huu wa likizo kama njia ya kujipatia kipato, na kwamba wote wawili watazikwa Alhamisi Mbalawala jijini Dodoma.
Hii si mara ya kwanza kutokea matukio ya wanafunzi kufukiwa na kifusi mkoani Dodoma ambapo Julai mwaka 2021 katika Kijiji cha Mbori kwenye Kata ya Matomondo wilayani Mpwapwa walifariki wanafunzi watatu wa darasa la nne na la tatu wakati wakichota mchanga.
Wanafunzi hao ilisemekana walikwenda kuchota mchanga na kokoto katika machimbo ya jirani wakiwa na wenzao wengine ambao walijeruhiwa, ingawa idadi yao haijajulikana.