Wanahabari watakiwa kutumia kalamu kupinga ukatili wa kijinsia
Muktasari:
Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kupaza sauti kuelimisha jamii kuachana na matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na wasichana.
Arusha. Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kupaza sauti kuelimisha jamii kuachana na matukio ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na wasichana.
Kauli hiyo imetolewa Novemba 25, 2021 na Mkufunzi Mwandamizi wa waandishi wa habari kutoka Shirika la Kimataifa la Internews, Alakok Mayombo katika mafunzo kwa wandishi wa habari yaliyotolewa kwa njia ya mtandao "Zoom".
Mafunzo hayo yalihusu kuandika habari za kupinga ukatili wa kijinsia, katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga vitendo hivyo vya kikatili.
Alisema mwaka huu kampeni hiyo ya kupinga ukatili wa kijinsia inatimiza miaka 30 na kuwa vyombo vya habari kwa kjjutumia kalamu zao wanaweza kuleta matunda na mabadiliko katika jamii juu ya vitendo hivyo.
"Vyombo vya habari kwa kutumia kalamu zetu tunaweza kuleta matunda kwa kupaza sauti ili jamii kuachana na vitendo vya kikatili ikiwemo mila na desturi potofu,"alisema
Naye moja ya wawezeshaji wa mafunzo hayo, Musa Juma alisema waandishi wa habari ni wadau muhimu na wana nafasi ya kuongeza uelewa kuhusu ukatili wa wanawake na wasichana.
"Tuna fursa ya kubadili mitazamo katika jamii juu ya masuala ya ukatili kwani katika maeneo mengine wanawake wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia lakini hawajui kama ni ukatili,"
Alisema vyombo vya habari vina wajibu wa kutoa fursa sawa katika kuwapa sauti wanawake katika habari zao.
"Sasa hivi ukatili mwingine mkubwa unaoendelea katika jamii ni udhalilishwaji wa wanawake kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, hivyo tuna wajibu wa kuelimisha jamii na kupinga vitendo hivyo vinavyoathiri wanawake wengi,"aliongeza
Naye Sultan Ali aliwakumbusha wanahabari kuhakikisha wanafichua na kuripoti masuala ya ukatili wa kijinsia na kuleta matokeo chanya (mabadiliko) katika jamii.