Wanaharakati wampinga Dk Ndumbaro elimu ya Katiba

Muktasari:
- Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na Jukwaa la Katiba (JUKATA) wamepinga msimamo huo wa Waziri Ndumbaro wa kutoa elimu ya Katiba kwa miaka mitatu.
Dar es Salaam. Baadhi ya wanaharakati wa Katiba na haki za binadamuwamekosoa kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria Dk Damas Ndumbaro aliyetangaza kuanza kwa utoaji wa elimu ya Katiba kwa miaka mitatu, wakisema waziri huyo analenga kuchelewesha mchakato huo.
Waziri Ndumbaro alitoa kauli hiyo jana katika mkutano wa wadau wa sheria ikiwemo mawaziri wastaafu wa Katiba na Sheria uliyofanyika Jijini Dar es Salaam, akisema kwa utafiti walioufanya imeonekana kuwa zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania hawaifahamu Katiba na wengine hata hawajawahi kuiona.
Leo Agosti 29 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) na Jukwaa la Katiba (JUKATA) wamekutana na waandishi wa habari na kupinga msimamo huo wa Waziri Ndumbaro.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa LHRC, Anna Henga amesema kauli ya Waziri Ndumbaro haina tija katika kufikia malengo ya Watanzania pamoja na nia ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kupata katiba mpya.
Amesema baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, alionesha nia ya wazi ya kurejesha mchakato wa katiba ili kutimiza azma yake ya 4R yaani (Mabadiliko) Reform, Reconciliation (Mapatano), Rebuild (Kujenga upya) and Resilience (Uthabiti).
“Matarajio yetu na ya Watanzania walio wengi tulitegemea kuona jitihada mahususi za kurekebisha dosari zilijitokeza na kusababisha kukwama kwa mchako wa katiba mwaka 2014 kwa kukosa mwafaka wa kitaifa,” amesema.
Akizungumzia utoaji wa elimu ulioelezwa na Waziri Ndumbaro, Henga amesema muda wa kuandaa katiba hadi ipatikane na kutumika sio chaini ya miaka mitano.
“Hivyo tukisema tutumie miaka mitatu kutoa elimu ya katiba alafu ndio mchakato uanze baadaye, itapelekea kuanza mchakato wa Katiba Mpya miaka minne ijayo na kupelekea kufika tena kwenye uchaguzi wa 2030 bila katiba mpya na wakati
hatujui nia na mtazamo wa kiongozi atakayekuja kuwa mrithi wa Rais Samia,” amesema.
Mbali na kupoteza muda, alisema utoaji huo wa elimu unatumia fedha nyingi ambazo zingeweza kukamilisha mchakato wa Katiba.
“Pesa hizi zitumie kuanzisha mijadala ya namna gani tunaweza anza mchakato wa katiba ambao ni shirikishi na waharaka. Elimu ya katiba mpya ilishatolewa na Tume ya Jaji Warioba pamoja na Bunge la Katiba,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba, Ananilea Nkya amewataka wasaidizi wa Rais kuwezesha kukamilika kwa mchakato huo.
“Hata chama kilichopo madarakani, kama kinataka kumsaidia Rais wa awamu ya sita, aweze kuiweka Tanzania katika hali nzuri, wahakikishe wanakuwa wa kwanza kusimamia Serikali Katiba ipatikane haraka iwezekanavyo,” amesema.
Naye Mkurugenzi wa jukwaa hilo, Bob Wangwe amesema kitendo cha Serikali kutumia Sh9 bilioni ni kupoteza rasilimali za wananchi.
“Utoaji wa elimu uliozungumzwziwa na Waziri ni kutaka kupoteza muda, ni kutaka kupoteza rasilimali za wananchi. Leo unapochukua Sh9 bilioni unaziweka kwenye mchakato ambao umeshafanyika, ni kukosa huruma na wananchi,” amesema.