Wanakijiji wamtuhumu mwenyekiti wao kuwapora ardhi

Muktasari:

  • Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Mgera, Kata ya Kiwele Wilayani Iringa wamedai wameporwa ardhi na mwenyekiti wa kijiji  na anawatishia amani.

Iringa. Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Hassan Moyo ameingilia kati mgogoro wa ardhi kati ya wakazi wa Kijiji cha Mgera Kata ya Kiwele, Wilayani Iringa na Mwenyekiti wa kijiji hicho, Lucas Mgata kwa kuzuia shughuli yoyote isifanyike katika eneo hilo hadi watakapopata ufumbuzi.

Wanakijiji hao wakiwemo wazee wawili Veronica Chusi (84) na Lusia Mbugano (90) wamemtuhumu mwenyekiti huyo kwa kupora kimabavu ardhi yao huku akiwatishia wale watakaodiriki kutoa taarifa  kwa uongozi wa juu.

Wakizungumza katika mkutano wa kijiji, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamesema  licha ya kuporwa ardhi, mwenyekiti huyo amekuwa akiwaongoza kimabavu kinyume cha sheria.

Chusi amesema mwenyekiti huyo amempora ardhi yake ambayo awali aliazima akidai anataka kufanya kilimo cha mazao lakini baadae akaifanya yake.

 “Nimeanza kutumia ardhi hii kabla ya mwenyekiti huyu hajazaliwa sasa iweje leo aseme ya kwake? Ardhi hii nilirithishwa na wazazi wangu,” amesema.

Chusi amesema kibaya zaidi ni kwamba, akienda kulalamika kwenye uongozi mwingine, amekuwa akitishiwa jambo ambalo alimuomba mkuu wa wilaya kuingilia kati.

"Tuna miaka zaidi ya themanini tunategemea ardhi hii, huyu ni mtoto mdogo sana,” amesema.

Lusia Mbugano (90) amesema kuwa mwenyekiti huyo amekuwa akiwanyang’anya ardhi mara kwa mara na walikuwa wanakaa kimya kwa kile walichodai alikuwa akiwatishia amani.

“Mara ya kwanza alitupora ardhi ambayo tuliachiwa urithi na marehemu baba yetu Mzee Mwesimpya Nyaulingo miaka ya 1937,” amesema.

Naye Ayubu Mtweve amemtuhumu mwenyekiti huyo kumpora ardhi yenye ukubwa wa ekari mbili anazomiliki kwa zaidi ya miaka 30.

Amesema alijaribu kulalamika kuhusu jambo hilo lakini hakukuwa na hatua yoyote iliyochukuliwa.

"Anapora ardhi kimabavu halafu ukianza kufuatilia anatishia kukuua na kukuweka ndani, sisi tumechoka tunaomba Mkuu wa wilaya leo utusaidie,” amesema Mtweve.

Akijibu tuhuma hizo, mwenyekiti huyo wa Mgera, Mgata amesema sio za kweli na wananchi hao wanamsingizia kutokana na utendaji wake wa kazi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Moyo amesema atatuma wataalamu kuchunguza malalamiko ya wananchi wa kijiji hicho na kuyashughulikia.

Mkuu huyo wa wilaya amepiga marufuku kazi yoyote kufanyika kwenye eneo hilo mpaka suluhisho litakapo patikana.