Wananachi watakiwa kuijali miradi ya Serikali

Wananachi watakiwa kuijali miradi ya Serikali

Muktasari:

Watanzania wamehamasishwa kuithamini na kuijali miradi ya Serikali inayojengwa katika maeneo yao.


Kongwa. Watanzania wamehamasishwa kuithamini na kuijali miradi ya Serikali inayojengwa katika maeneo yao.

Wito huo umetolewa leo Jumamosi Novemba 28,2020 na ofisa uhamasishaji na mahusiano wa Shirika lisilo la kiserikali la Raleigh Tanzania’s, Peter Lazaro wakati akikabidhi mradi wa ukarabati na uingizaji maji katika zahanati ya kijiji cha Mseta wilaya ya Kongwa.

Raleigh Tanzania’s kupitia mradi wao wa Social Accountability Youth (SAY) wanatekeleza miradi ya uwajibikaji kwa jamii wakishirikiana na Shirika la Simavi  katika mradi wa Mkaja unaosambaza maji na kukarabati kituo cha afya Mseta.

Lazaro amesema watu wengi vijijini wamekuwa na utamaduni wa kutojali miradi ya serikali ikiwemo majengo na kuwataka kubadilika.

Ofisa huyo amesema shirika hilo limeamua kutoa elimu hiyo na kuwahamasisha watu wathamini miradi hiyo kwa kuwa inajengwa na kufanya kazi kwa ajili ya faida yao, “mradi wetu umewanufaisha wakazi wa Mseta na vitongoji vyake, lakini tunalenga jamii iwe na mtazamo chanya katika kuithamini na kuitunza miradi ambayo wamepelekewa na serikali au na mashirika.”

Ofisa mtendaji wa kijiji cha Mseta, Ezekiel Mlugu  amesema mabadiliko yaliyofanywa na wakazi wa eneo hilo katika kipindi kifupi, yametokana na elimu waliyoipata kutoka katika shirika hilo iliyosaidia kuifufua miradi ya Serikali.