Wananchi Kilimanjaro wamlilia Mgwhira

Muktasari:

  • Ni huzuni isiyokuwa na kifani kutokea kwa kifo cha aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira hivyo ndivyo unavyoweza kusema.

Moshi. Ni huzuni isiyokuwa na kifani kutokea kwa kifo cha aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira hivyo ndivyo unavyoweza kusema.


Wananchi wa mkoani Kilimanjaro wameonekana makundi kwa makundi wengine wakiwa wameshika tama wakiwa hawaamini kama Mghwira amefariki dunia.

Mghwira ambaye alikuwa amelazwa katika Hospitali ya Nkoaranga kwa tatizo la kupumua na baadaye kuhamishwa katika Hospitali ya Mount Meru Jijini Arusha amefariki leo mchana baada ya hali yake kubadilika gafla.

Wakizungumza kwa masikitiko makubwa wananchi wa mkoa huo wamesema kifo cha mama Mghwira ni pigo kubwa kwani alikuwa ni mtu mwenye upendo na msikivu kwa watu wote.


Elizabeth Joseph mkazi wa Mji wa Moshi amesema kuwa mpaka sasa haamini kilichotokea kwa mama Mghwira huku akisema kifo chake kimekuwa ni pigo kubwa  kwani alikuwa ni mwanamke mwenye maono ya mbali.

"Tumeshtushwa sana na kifo cha mama yetu mpendwa Mghwira kweli ameondoka katika kipindi ambacho Taifa likiwa linamtegemea, amekuwa ni mama mwenye upendo na ambaye alikuwa na maono ya mbali, alikuwa ni mama mwenye uthubutu alikuwa ni mama mpambanaji, kifo chake kitaacha alama kwenye mioyo yetu,"


"Tutamkumbuka Mghwira kwa mengi tuliishi naye hapa Kilimanajro kwa upendo mkubwa alikuwa akimsikiliza kila mtu sio mkubwa wala sio mdogo, hata alipostaafu wananchi wa Kilimanajro tuliumia sana, kazi ya Mungu haina makosa tutamkumba kwa mengi, Mwenyezi Mungu ampe pumziko la milele,"Anna Temba Mkazi wa Moshi Mjini.


Winie Shao mmoja wa wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro amesema atamkumbuka mama Mghwira kwani alikuwa ni mtu wa watu na mwenye upendo kwa kila mtu na kuwajali wananchi wake wakati wa uongozi wake.


"Kifo cha mama Mghwira kimetuumiza sana wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro, alikuwa ni mama wa mfano wakati mwingine aliweza kutatua migogoro ya wanandoa pale ambapo kuna ulazima, alikuwa ni mtu ambaye hapendi migogoro yuko tayari atenge muda wake baada ya kazi kusikiliza kero za wananchi wake,"amesema Winie.

Robert Kalisti ambaye ni mkazi wa Majengo amesema mama Mghwira alikuwa sio mtu wa siasa alikuwa ni mtekelezaji na kwamba aliwahudumia wananchi wake bila ubaguzi wowote.

"Mama Mghwira alikuwa ni mama wa mfano hapa Kilimanajro alikuwa akiwasaidia wananchi wake bila kujali itikadi zao za kisiasa wala dini, ametusaidia sana mama Mghwira na hata alipondoka hapa Kilimanajro alituachia pengo kubwa ambalo kuzibika kwake ni ngumu, alikuwa ni mama wa watu,ndio maana kila mahali ukipita sasa hivi Mkoa wa Kilimanjaro kila mtu anamlilia, kwa kweli alikuwa ni mama wa mfano, tunamwombea kwa Mungu apumzike kwa amani,"