Wananchi Kiteto watoa ekari 5 ujenzi kituo cha Polisi

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara,RPC George Katabazi akiwahakikishia wananchi wa Olengasho Kata ya Partimbo Kiteto waliotoa eneo la kujenga kituo kidogo cha Polisi kuwa ameridhia na atatoa ushirikiano wa ujenzi huo Picha na Mohamed Hamad Kiteto

Muktasari:

  • Wadai kukamilika kituo hicho wataepuka kutembea kilometa 40 kwenda na kurudi kusaka huduma hiyo Kibaya.

Kteto. Wananchi wa Olengasho, Kijiji cha Kimana wilayani Kiteto mkoani Manyara, wametoa eneo la ekari 5, kwa ajili ya ujenzi wa Kituo kidogo cha Polisi, Kata ya Partimbo ambayo inakabiliwa na migogoro ya ardhi baina ya wakulima na wafugaji kila mara.

Kituo hicho kupunguza adha ya wananchi kusaka huduma hiyo kiliometa 40 kwenda Kibaya na kurudi ambako ni makao makuu ya wilaya ya wilaya ya Kiteto yalipo.

Wakimweleza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Manyara, RPC George Katabazi, Machi 2, 2023 wananchi hao wamesema tatizo linalowakabili ni kutokuwa na usalama katika maeneo hayo kutokana na mwingiliano wa watu kutoka maeneo tofauti waliofika kwa shughuli za kiuchumi.

"Mtanzania yoyote ana haki ya kuishi popote kwa mujibu wa sheria ili mradi asivunje sheria, sasa hapa usalama wetu ni mdogo tunahitaji kuwa na kituo cha Polisi ili kulinda raia na mali zetu.

"Wananchi tumetoa ekari tano za kujenga kituo na nyumba ya askari na hii itapunguza  changamoto inayotukabili na viongozi, hivyo kutokana na ukubwa wa tatizo hilo Kamanda Katabazi tunaomba msaada wako kuridhia," amesema mkazi wa eneo hilo Mariamu Isa.

Kufuatia hali hiyo wananchi hao wamemwomba Kamanda Katabazi kuridhia eneo hilo la ekari 5 lijengwe kituo kidogo cha Polisi ili kuondoa adha wanayopata kusaka huduma hiyo km 40 kwenda makao makuu ya Wilaya ya Kiteto yalipo mjini Kibaya.

"Huku kwetu kuna vibaka wengi sana, waume zetu nao pia ni changamoto, ng'ombe za Wamasai ni tatizo zinakula mazao yetu wakati wote usiku na mchana, mwanamke ukiongea tu huko mashambani ni kipigo cha hali ya juu hivyo kujengwa kituo hiki kidogo cha Polisi kitatusaidia haswa wanawake," alisema Mariamu.

"Kwa sasa hali iliyopo tunahitaji kituo cha polisi, wananchi wametoa sehemu ya maeneo yao kwa ajili ya ujenzi, Kamanda wa Polisi tunaomba msaada wa kukubaliwa kuendeleza ujenzi huu ili kuondoa adha wanayopatawananchi," amesema Mwanaidi Mdugi  ambaye ni Ofisa Mtendaji Kijiji cha Kimana.

"Wananchi wako tayari kutoa maeneo yao na hata ofisi ya muda ya Polisi tunaomba kupatiwa pia Askari Kata awe hapa ili tuweze kupata huduma hii wakati mchakato wa ujenzi unaendea," amesema Paulo Tunyoni Diwani Kata ya Partimbo.

Wananchi hao walitumia nafasi hiyo kwenda kumuonyesha RPC Katabazi eneo hilo la ekari 5 na kusema yuko tayari kuunga mkono jitihada hizo.

Mwenyekiti wa eneo hilo la Olengasho, Safari Feo amedhibitisha eneo hilo la ekari tano kwa kumwonyesha Kamanda Katabazi ambaye amesema linatosha kwa kituo na nyumba ya askari.

"Ni kweli tumeshuhudia eneo ambalo linafaa kwa ukubwa ni ekari 5, zinatosha ujenzi wa kituo kitogo cha Polisi pamoja na makazi ya Askari wetu," amesema.