Wananchi Marangu wamkumbuka Mrema

Aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha TLP, Agustino Mrema
Muktasari:
- Mrema (77) aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, alifariki dunia leo Jumapili, Agosti 21, 2022, asubuhi, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
Moshi. Baadhi ya wakazi wa kijiji cha Kiraracha, Marangu mkoani Kilimanjaro ambako alizaliwa aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha TLP, Agustino Mrema wamemuelezea mwanasiasa huyo kuwa alikuwa mkarimu, mpatanishi na mcha Mungu.
Wakizungumza na Mwananchi leo Jumapili Agosti 21, 2022 wamesema kuwa wamepoteza mtu muhimu katika kuleta maendeleo.
Mrema (77) aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, amefariki dunia leo Jumapili, Agosti 21, 2022, asubuhi, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam.
Mkazi wa kijiji hicho, Emiliana Joachimu amesema "Mrema alikua mtu mkarimu, mwenye upendo kwa watu, alikua mpatanishi, mtu akiachana na mwenza wake hata miaka miwili atawatafuta na kuwapatanisha"
Mary Ngowi ameeleza kuwa kifo cha Mrema ni pigo kwani alikua ni msaada kwa familia na jamii iliyomzunguka.
"Alikua mkarimu sana, ukiwa na shida ukimweleza anakusaidia, tunaishia kusema maisha ni fumbo kwani hatuamini kama kweli amekufa,
"Amewasaidia watu wengi sana, ukiwa na shida ukimweleza anakusaidia iwe ni fedha au ugomvi, alikua anatoa misaada kanisani, shuleni, barabara ni yeye alisababisha hadi sasa kuna usafiri wa uhakika eneo hili, tutamkumbuka kwa mengi” amesema Mary.
Mdogo wa Mwanasiasa huyo, Michael Mrema amesema kifo cha kaka yake ni pigo kwa familia kwani alikua ndiye kaka mkubwa katika familia hiyo.
"Kuna ndugu yangu mmoja anaishi Chanika Dar es Salaam siku tatu hivi zimepita, alinieleza kuwa hali yake imebadilika, na amepelekwa Muhimbili yupo kwenye oksijeni lakini baada ya muda hali yake iliimarika na tukaendelea kuongea naye mpaka jana jioni" amesema
Michael amesema amesema kuwa kaka yake alikuwa anasumbuliwa na tatizo la kisukari, presha pamoja na ugonjwa wa ngozi kwa muda mrefu.
Theresia Michael Mrema ambaye ni shemeji wa marehemu, amesema kuwa wamepokea kifo hicho kwa masikitiko makubwa.