Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi Maswa walia shida ya maji

Hiki ni moja ya kisima cha maji katika kijiji cha Sulu Wilaya ya Maswa. Picha na Samwel Mwanga

Muktasari:

  • Wananchi wa Kijiji cha Sulu wilayani Maswa mkoani Simiyu wanaendelea kukabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama baada ya mradi wa maji uliokuwa ukitoa huduma kusitisha uendeshaji wake licha ya kuwepo kwa miundombinu.

Maswa. Wananchi wa Kijiji cha Sulu wilayani Maswa mkoani Simiyu wamelazimika kuendelea kutumia maji yasiyo safi na salama kutoka kwenye visima vya kienyeji na mabwawa, hali inayohatarisha afya zao.

Hali hiyo imetokana na kusimama kwa huduma ya mradi wa maji uliokuwa ukihudumia kijiji hicho, licha ya kuwepo kwa miundombinu yake, hali iliyosababisha wakazi kutumia vyanzo visivyo salama vya maji.

Kutokana na hali hiyo, wananchi wamelazimika kutumia maji kutoka mabwawa na visima vya asili ambavyo hutumiwa pia na mifugo, jambo linaloongeza hofu ya kuibuka kwa magonjwa ya mlipuko.

Wakizungumza leo Mei 13, 2026 kwa nyakati tofauti, baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wamesema wamekuwa wakipata mateso kutokana na kutumia muda mwingi kutafuta maji.

Maria Shija, mkazi wa kijiji hicho, amesema hapo awali walikuwa wakipata huduma ya maji ya bomba, lakini sasa ni zaidi ya mwaka mmoja wamekosa huduma hiyo.

“Maji yaliyokuwa yakitoka kwenye mabomba yalitusaidia sana, lakini sasa hakuna kabisa. Tunachota maji kwenye mabwawa ambayo hata mifugo hutumia,” alisema.

Naye John Ndege amesema ukosefu wa maji umeathiri afya za wananchi na shughuli zao za kila siku, huku akiiomba serikali kuchukua hatua za haraka.

Joseph JIlala mkazi wa kijiji cha Sulu akichota maji katika moja ya visima vilivyoko kijijini hapo lakini maji hayo si safi na salama. Picha na Samwel Mwanga

“Wanawake na watoto ndiyo wanaoteseka zaidi kwa kutafuta maji umbali mrefu. Tunaomba serikali ituangalie kwa haraka,” alisema.

Kwa upande wake, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Ruwasa) wilayani Maswa, Mhandisi Salum Masaka, amesema awali mradi huo ulikuwa ukitegemea chanzo cha maji kutoka kijiji jirani cha Mbaragane, ambacho kilikauka.

Amesema baada ya chanzo hicho kushindwa, Ruwasa ilianza kutafuta chanzo kipya ndani ya Kijiji cha Sulu, ambapo mkandarasi STRATON Co Ltd alipatikana kwa gharama ya Sh619.8 milioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo.

Hata hivyo, amesema utekelezaji wa mradi umesimama kwa sasa kutokana na mkandarasi kutolipwa fedha kutoka serikalini.

Diwani wa Kata ya Mbaragane, Abel Masunga, amesema changamoto ya maji imeendelea kuwa kubwa na kuathiri maisha ya wananchi wa eneo hilo.

Amesisitiza umuhimu wa Serikali kutoa fedha kwa wakati ili mradi ukamilike na wananchi waanze kupata huduma ya maji safi na salama.

“Wananchi wanapata shida kubwa kutokana na ukosefu wa maji. Serikali ikitoa fedha mapema mradi utakamilika na tatizo litapungua,” amesema.