Wananchi Monduli wahimizwa kuvuna maji ya mvua
Mkurugenzi Mtendaji wa Vijana Assembly, Mbayani Tayai Lengima (akiwa amevaa shati jeupe), akikabidhi vifaa vya kuvuna maji Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Kisioki Moitiko, kwa ajili ya ugawaji kwa kaya zenye uhitaji wakati wa uzinduzi wa mradi huo. Picha na Bertha Ismail
Muktasari:
- Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Kisioki Moitiko wakati wa uzinduzi wa mradi wa ugawaji wa matenki ya maji na gata unaofadhiliwa na shirika la Vijana Assembly kwa ajili ya kusaidia uvunaji wa maji katika kaya, tukio lililofanyika katika kata ya Sepeko.
Arusha. Wakazi wa Wilaya ya Monduli mkoani Arusha wamehimizwa kuchukua hatua za dharura kwa kuwekeza katika miundombinu ya uvunaji wa maji ya mvua ili kukabiliana na ukame unaoendelea kuathiri maisha na usalama wa chakula.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Kisioki Moitiko, wakati wa uzinduzi wa mradi wa ugawaji wa matenki ya maji na gata unaofadhiliwa na shirika la Vijana Assembly, hafla iliyofanyika katika kata ya Sepeko.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vijana Assembly, Mbayani Tayai Lengima (akiwa amevaa shati jeupe), akikabidhi vifaa vya kuvuna maji Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Kisioki Moitiko, kwa ajili ya ugawaji kwa kaya zenye uhitaji wakati wa uzinduzi wa mradi huo. Picha na Bertha Ismail
Amesema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha mvua kuchelewa na mabwawa mengi kukauka, hali inayosababisha uhaba mkubwa wa maji kwa matumizi ya binadamu na mifugo. Kutokana na hali hiyo, amewataka wananchi kujenga mifumo ya uvunaji wa maji ikiwemo matenki, gata na mifumo ya kuvuna maji kutoka kwenye paa za nyumba.
Moitiko amesema uvunaji wa maji si chaguo tena bali ni hatua muhimu ya kukabiliana na ukame unaojirudia mara kwa mara, huku akiwahimiza wananchi kuchukua fursa ya mvua zinazotarajiwa kunyesha Februari ili kuhifadhi maji ya kutosha.
Ametumia nafasi hiyo kulishukuru shirika la Vijana Assembly kwa kujitolea kusaidia kaya zenye uhitaji mkubwa kupitia ugawaji wa matenki na gata, hatua itakayosaidia jamii kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Vijana Assembly, Mbayani Tayai Lengima, amesema mradi huo ni sehemu ya mpango wa kukabiliana na uhaba wa maji vijijini, ambapo tayari matenki 15 ya lita 5,000 yamegawiwa, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kugawa matenki 200 mwaka huu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Vijana Assembly, Mbayani Tayai Lengima (akiwa amevaa shati jeupe), akikabidhi vifaa vya kuvuna maji Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Kisioki Moitiko, kwa ajili ya ugawaji kwa kaya zenye uhitaji wakati wa uzinduzi wa mradi huo. Picha na Bertha Ismail
Mmoja wa wanufaika, Ibrahim Leiyo, amesema uhaba wa maji umeathiri kwa kiasi kikubwa maisha ya wakazi wa vijiji kadhaa wilayani humo, huku wananchi wakilazimika kununua maji kwa gharama kubwa, hali inayoongeza mzigo wa maisha.
Aidha, mkazi wa Sepeko, Nariku Ashumu, amesema ukame umeongeza mateso kwa wananchi wanaotembea umbali mrefu kutafuta maji, na kuiomba Serikali pamoja na wadau wengine kuongeza jitihada za kusaidia jamii kupata miundombinu ya kudumu ya uvunaji wa maji.