Wananchi Mwanga walalamikia uhaba nyumba za watumishi wa afya
Mbunge wa Jimbo la Mwanga, Dk Ngwaru Maghembe akizungumza na wananchi wa kata ya Kirya, katika mkutano wa hadhara ambao umefanyika leo katika kata hiyo. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Licha ya kuwapo kwa zahanati na vituo vya afya ukosefu wa nyumba za wahudumu wa afya umekuwa changamoto kwa wananchi kupata huduma za afya muda wote.
Mwanga. Baadhi ya wananchi wa kata za Kirya, Kilomeni na Lembeni, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro wamelalamikia ukosefu wa nyumba za wahudumu wa afya katika baadhi ya zahanati, hali inayosababisha kukosekana kwa huduma za dharura nyakati za usiku.
Wamesema huduma hukosekana kutokana na wahudumu hao kuishi mbali na zahanati na vituo vya afya wanavyohudumu.
Wakizungumza leo Jumapili, Februari 22, 2026 katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na Mbunge wa Mwanga (CCM), Dk Ngwaru Maghembe wananchi hao wamesema changamoto hiyo imekuwa ikiathiri upatikanaji wa huduma kwa wagonjwa wanaougua nyakati za usiku, hivyo kuiomba Serikali kuchukua hatua za haraka ili kuhakikisha huduma zinapatikana wakati wote.
Mmoja wa wananchi wa kata ya Kirya, Grace Mdee amesema wahudumu wa afya kuishi mbali na vituo vyao vya kazi baadhi ya ndugu wamepoteza wapendwa wao kwa kukosa huduma za dharura nyakati za usiku.
"Mheshimiwa Mbunge, zahanati zetu hazina nyumba za wauguzi, wanakaa mbali nazo, hivyo sisi wananchi tunashindwa hata kuwapeleka wagonjwa usiku tukihofia kukosa huduma.
“Unaweza kumpeleka mgonjwa usiku lakini humkuti muhudumu kwenye zahanati kwa sababu wamepanga mbali na vituo vyao vya kazi," amesema Grace.
Mwananchi huyo, ameiomba Serikali kuona umuhimu wa kujenga nyumba za wahudumu wa afya karibu na vituo vyao vya kutolea huduma za afya ili kunusuru maisha ya wananchi.
Mwananchi mwingine, Jonas Mashambo, amesema kukosekana kwa huduma za afya nyakati za usiku kunawapa changamoto kubwa wananchi kwa kuwa ndugu anapoumwa ghafla nyakati za usiku inakuwa ngumu kumpeleka kupata huduma ya haraka kwani hakuna wahudumu.
"Juzi kati mke wangu aliugua ghafla usiku, nikawaza zahanati yetu hapa haina wahudumu usiku, bahati nzuri ndio kulikuwa kunakucha nikamwandaa harakaharaka huku nikimwomba Mungu kukuche mapema, kweli kilikucha nikampeleka kituoni akapata huduma," amesema Mashambo
"Ingekuwa ameugua saa nane usiku ningelia na nani maana zahanati zetu hazina wahudumu usiku na wanaishi mbali na hapa, tunaomba Serikali kwa moyo wa huruma iangalie namna inavyoweza kufanya kukabiliana na changamoto hii."
Mwananchi mwingine, Anorld Tengia, amesema pamoja na vituo hivyo kukosa wahudumu wa afya nyakati za usiku, baadhi ya majengo pia ni chakavu na hayajafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.
Baadhi ya wananchi wa kata za Kirya, Kilomeni na Lembeni, Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro wamelalamikia ukosefu wa nyumba za wahudumu wa afya katika baadhi ya zahanati, hali inayosababisha kukosekana kwa huduma za dharura nyakati za usiku.
Akijibu changamoto hizo, Dk Maghembe amewataka wananchi hao kuwa wavumilivu wakati suala hilo likifanyiwa kazi. Ambapo amesema Serikali ina mpango mzuri wa kuhakikisha wananchi wanapata huduma stahiki nyakati zote.
“Nimewasikiliza wananchi wangu na nimepokea kero zote na baadhi ya kero nitazipeleka katika mamlaka husika moja kwa moja kwa hatua zaidi,” amesema Dk Maghembe ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Pamoja na mambo mengine, amesema atahakikisha anaweka kipaumbele katika kuimarisha miundombinu ya barabara katika kata zote za wilaya hiyo ili kurahisisha huduma za kijamii na kiuchumi.
“Nitahakikisha changamoto hizi zote mlizozileta hapa zinapatiwa ufumbuzi wa haraka ili kuboresha huduma za kijamii na kuinua maendeleo ya wananchi wa Mwanga,” amesema Dk Maghembe.