Wananchi Nanyamba walia kero ya maji
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mkahara kata ya Kiyanga Halmashauri ya mji Nanyamba wakiongea jambo na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda (wa kwanza kushoto) alipotembelea kijijini hapo hivi karibuni. Picha na Florence Sanawa
Muktasari:
- Wakazi wa Kijiji cha Mkahara Halmashauri ya mji Nanyamba waomba mradi wa maji wa kisima ukamilike ili kuwaondolea adha wanayopata kwa sasa ambapo hulazimika kununua dumu kwa Sh1,000.
Mtwara. Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mkahara Kata ya Kiyanga, Halmashauri ya Mji wa Nanyamba wamemuomba Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mwanahamisi Munkunda awasidie kuharakisha kukamilika kwa mradi wa maji uliopo kijijini hapo ili kupunguza changamoto ya kufuata maji vijiji jirani ambapo huuziwa dumu moja la lita 20 kwa Sh1,000.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumapili Novemba 12, 2023 kijijini hapo Khadija Salum Ally amesema kuwa maji ni shida kijijini hapo ambapo hulazimika kwenda vijiji jirani kutafuta maji ama kununua dumu moja kwa bei ya Sh1,000.
Amesema kuwa wanaotaabika kwa kiasi kikubwa ni wanawake na watoto ambao ndio wanatumia maji kwa kufua nguo na kupika ambapo mtoto hawezi kwenda shuleni akiwa mchafu.
“Maji ni shida tumeona kuna mradi hapa kijini kwetu tunaomba ukamilishwe haraka ili kutunusuru na kununua dumu kwa Sh1,000 na kutembea umbali mrefu na kwenda kijiji jirani cha kiyanga kufata maji” amesema Ally
Naye Mzee Chiwihi mkazi wa kijiji cha Mkahara amesema kuwa maji yanapatikana kwa shida na yanauzwa hivyo wananchi wasio na kipato hulazimika kutembea umbali mrefu kufata maji vijiji jirani.
“Yaani huwezi oga huwezi fua nguo zikataka kwa maji ya kununua 1000 ama utembee zaidi ya kilomita tatu alafu uje ufulie maji yaote hii haiwezekani tunaomba serikali isikie kilio chetu”
Juma Omary mkazi wa kijiji cha Mkahara anasema kuwa kijij hiki kina eneo bondeni linapita mradi wa maji na tayari wameshatoboa maji shida kubwa pampu tunaomba tusaidiwe.
“Tunashida kubwa ya maji miundombinu ipo wametoboa bondeni shinda na pampu dumu tunanunua 1000 mtu mwenye familia kubwa anaishije tunaomba mradi huu ukamilike ili tupate maji” amesema Omary
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mwanahamisi Munkunda amewaambia wananchi hao kuwa amepokea kero hiyo na ataifanyia kazi kwa haraka kupitia mamlaka husika.
Akiongea kwa njia ya simu, Mbunge wa Nanyamba, Abdallah Chikota amesema kuwa katika kijiji hicho kulikuwa na kisima cha zamani ambacho kilikufa na pampu pia lakini serikali imechimba kisima kingine kirefu zaidi chenye maji mengi ambacho kikikamilika ,kitaondoa tatizo la maji katika kijiji hicho ambapo inasubiriwa pampu tu.
Hivi karibuni mkoa uliingia mkataba wa ujenzi wa miradi saba ya maji yenye thamani ya Sh9 bilioni ambapo Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijiji (Ruwasa) Mkoa wa Mtwara, Mhandisi Primy Damas alisema zaidi ya wananchi 65,000 watanufaika na miradi hiyo wakiwemo wa Nanyamba ambapo kwa sasa uputikanaji wa maji vijijini ni asilimia 67.