Wananchi Ngorongoro wadai kupunguziwa huduma, Serikali yajibu

Arusha. Wakati baadhi ya wananchi wanaoendelea kuishi ndani ya eneo la Hifadhi ya Ngorongoro wakilalamika kupunguziwa huduma za jamii, Serikali imesema madai hayo hayana ukweli.

Malalamiko hayo yanatolewa ikiwa mwaka mmoja umepita tangu Serikali ilipoanza utekelezaji wa mradi wa kuwahamisha kwa hiari wakazi wa eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na kuwapeleka kijiji cha Msomera, wilayani Handeni, Tanga. Utekelezaji ulianza Juni 6, mwaka jana.

Wananchi hao wanadai kuna punguzo katika utoaji huduma za afya na chakula, kutokarabatiwa miundombinu ya elimu, makazi na barabara.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro, Nassoro Shemzigwa alipotafutwa na Mwananchi kuzungumzia madai ya kusitishwa huduma za jamii alisema; “Tunafuatilia na huduma zinaendelea kutolewa.”

Diwani wa kata ya Alaitole, James Moringebakionyesha moja ya nyumba za watumishi zilizoharibika lakini hazijakarabatiwa

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Raymond Mangwala alisema huduma zinaendelea kama kawaida.

“Kimsingi huduma za afya zipo kama zilivyo, huduma za elimu zinaendelea kama kawaida hata shule ya sekondari iliyoongoza matokeo ya kidato cha sita (kiwilaya) inaitwa Embarway, nenda kwenye matokeo yatakuonyesha.

“Kwa hiyo, huduma za kijamii zinaendelea kama kawaida, hakuna huduma iliyosimama,” alisema.

Huduma za afya

Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina kwa kuwa si msemaji, mmoja wa viongozi wa kituo cha afya kata ya Enduleni kinachoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Kanisa Katoliki na Serikali, alisema huduma zilianza kudorora kabla ya utekelezaji wa mradi wa kuhamisha wananchi eneo hilo.

“Kwa ujumla bajeti ya mwaka ya kuendesha hospitali hii ni zaidi ya Sh1.2 bilioni, kati ya hizo, Sh300 milioni hutolewa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, lakini tangu maambukizi ya Uviko-19 fedha hizo zilisitishwa. Tulitarajia baada ya kuisha kwa maambukizi, fedha zingerudishwa lakini hadi leo hatupati,” alieleza.

Alisema fedha nyingine hutolewa kupitia mishahara ya watumishi wanaolipwa na Serikali na takribani Sh150 milioni huchangiwa na wagonjwa, huku kiasi kilichosalia hutolewa na kanisa.

“Kutokana na hali hiyo tumepunguza wafanyakazi 17 na kubakiwa na 22 ambao wanalazimika kuongeza muda wa kufanya kazi,” alisema na kuongeza kuwa changamoto ipo katika ufanyaji operesheni na kutoa huduma ya mama na mtoto.

Alisema mamlaka haitoi tena chakula kwa wagonjwa, bali ikiendelea na utoaji wa mafuta ya magari na kuyafanyia matengenezo.

Kwa upande wake, Londomono Elekaseye alidai kinamama hawapati huduma za afya ipasavyo kutokana na punguzo la utolewaji fedha.

“Kwa sasa pia haturuhusiwi kukata miti kwa ajili ya kukarabati nyumba, hivyo tunalala nje na ni hatari nyakati za usiku kwa sababu ya baridi na wanyama wakali,” alieleza.

Kwa upande wake, Moishikito Sangal alidai, “Huduma ya mama na mtoto imepunguzwa tofauti na zamani.”

Meneja Uhusiano wa Umma wa NCAA, Joyce Mgaya akizungumza na Mwananchi kwa simu kuhusu madai hayo alisema; “Hayo madai si ya kweli, sijaona popote ambako hatutoi huduma zote za jamii.”

Akizungumzia kuondolewa kwa Sh300 milioni kwa kituo cha afya, Mgaya alisema awali utaratibu wa fedha ulikuwa wa mamlaka kujipangia matumizi yake.

“Tulikuwa tunakusanya fedha, tunajipangia matumizi, lakini sasa tuko kwenye utaratibu wa kuomba fedha serikalini kama taasisi nyingine za umma kwa maana ya kupokea OC. Kwa hiyo, tunaomba fedha kwa ajili ya matumizi ya wenyeji.

“Kipindi cha Uviko-19 tulikuwa tunapewa fedha na Serikali, biashara ya utalii iliathirika sana, hivyo Serikali ilikuwa inatoa fedha za kutuwezesha shughuli za utalii. Utaratibu huohuo unaendelea kutumika mpaka leo, kwa hiyo ukisema hatutoi huduma mimi sijaona,” alisema.

Elimu

Wananchi wanalalamika shule zina hali mbaya, baadhi ya majengo yaliezuliwa na upepo na madarasa yana nyufa lakini hayajakarabatiwa.

Miongoni mwa shule hizo ni ya msingi Ndian ambayo madarasa yako hatarini kuanguka kutokana na nyufa kama anavyoeleza Lazaro Mringet, mkazi wa kijiji cha Nasporio.

Alisema uongozi wa kijiji ulishamwandikia barua mtendaji wa kata, ofisa elimu wa kata, mkurugenzi wa Halmashauri ya Ngorongoro na diwani ambaye pia ni mbunge ili kushughulikia changamoto hiyo.

Hata hivyo, mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Shemzigwa alipoulizwa kuhusu hilo alisema, “hatuna hizo taarifa.”

Diwani wa Alaitole, James Moringe, alisema miundombinu ya shule imechakaa na kuharibika, huku wakizuiwa kuikarabati.

“Tumepata changamoto, shule hazina vyoo wala madarasa ya kutosha na hospitali hazina wahudumu na huduma za kutosha, lakini fedha zipo kwenye akaunti hazifanyi kazi za kusaidia wananchi.

“Kwa mfano shule ya msingi Enduleni yenye watoto 1,904 haina choo bora, kuna upungufu wa matundu 49, yaliyopo ni tisa, manne ya wavulana na matano ya wasichana, yamejaa na haturuhusiwi kukarabati wala kupitisha vifaa kule getini,” alisema.

Aliitaja shule ya sekondari ya wasichana Iseye, akisema ina matundu matano ya vyoo ambavyo vimejaa na hawana bwalo, hivyo wanakula chakula nje. Pia alilalamika kwamba barabara hazijafanyiwa ukarabati.

Chakula

Kuhusu chakula, diwani huyo alisema uingizwaji wa chakula umekuwa wa shida na wao wanazuiwa kulima.

Alidai awali NCCA ilikuwa ikitoa chakula kwa watoto kwa shule za msingi, lakini sasa wamesitisha.

Akizungumzia uharibifu wa miundombinu, Mgaya alisema; “Kitu kinachokataliwa ni ujenzi wa miundombinu mipya, lakini si ukarabati.

“Kwa majengo yote yaliyopo, wakitoa taarifa sehemu sahihi na wakatoa maelezo nini kinachotakiwa kufanyika wanapewa vibali kulingana na utaratibu.”

Kuhusu ukarabati wa barabara ambao pia unalalamikiwa na wananchi alisema; “kati ya maeneo tunayojitahidi kufanya vizuri ni upande wa barabara.

“Serikali ilitupa zaidi ya Sh6 bilioni kununua vifaa kwa maana ya magreda na mitambo kwa ajili ya kurekebisha barabara, kwa hiyo mtu akisema barabara hazijatengenezwa naweza kumkukatalia.”

Kuhusu huduma ya chakula, Mgaya alisema; “chakula walikataa wenyewe, tulikuwa tunaleta wao wakasema hapana. Kilikuwa ni chakula cha kujikimu.”

Dondoo

Kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuhusu Mashirika ya Umma ya mwaka wa fedha wa 2021/22, tangu mradi ulipoanza Juni 6, 2022 hadi Oktoba 19, 2022, jumla ya kaya 407 (asilimia 1.85) zenye jumla ya watu 2,125 (asilimia 1.93) na mifugo 11,490 (asilimia 1.53) zilikuwa zimehamishwa na kupewa makazi katika Kijiji cha Msomera, wilayani Handeni Mkoa wa Tanga.