Wananchi Serengeti waomba operesheni dhidi ya majambazi

Diwani wa Majimoto wilayani Serengeti, Johannes Masirori akizungumza kuhusu kuliomba jeshi la polisi kufanya operesheni endelevu kuzuia uhalifu. Picha na Beldina Nyakeke

Muktasari:

Baadhi ya wakazi wa wilaya ya Serengeti mkoani Mara wameliomba Jeshi la Polisi mkoani humo kufanya operesheni za mara kwa mara katika maeneo yao ili kuimarisha hali ya ulinzi dhidi ya wahalifu.

Serengeti. Wakati baadhi ya wananchi wakitaka uchunguzi ufanyike kwa mauaji ya watu watatu wanaodaiwa kuwa majambazi wilayani Serengeti Mkoa wa Mara, baadhi ya wananchi wameliomba Jeshi la Polisi mkoani humo kuongeza operesheni kama hizo.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mara, Longinus Tibishiwanu, Polisi wa mkoa huo wakishirikiana na wenzao wa Mwanza, Simiyu na Tarime- Rorya waliwauwa kwa kuwapiga risasi watu watatu kwa madai ya kujihusisha na ujambazi katika wilaya za Butiama na Serengeti.

Waliouwawa katika tukio hilo ni pamoja Mairo Togoro (56) mkazi wa kijiji cha Majimoto, Mwise Simon (54) mkazi wa kijiji Nyamihuru na Mugare Mokiri mkazi wa kijiji cha Nyamikobiti wote wa wilaya ya Serengeti.

Miongoni mwa wanaotaka uchunguzi ufanyike kwa mauaji hayo ni Katibu wa Baraza la Wanawake wa Chadema, Catharine Ruge ambaye ni mpwa wa mmoja wa watu waliouwawa, akisema wanakusudia kufungua kesi ili kufanyika uchunguzi huo.

Hata hivyo, wakizungumza leo Septemba 26, baadhi ya wanachi wamesema operesheni hizo zitasaidia kupunguza uhalifu.

Diwani wa Majimoto ambapo ndipo tukio la mauji lilipotekea, Johannes Masirori amesema kuwa matukio ya ujambazi yamekuwa yakitokea katika maeneo yao hali ambayo imekuwa ikizua hofu.

"Siku za hivi karibuni matukio mengi yamekuwa yakijitokeza hivyo kusababisha watu kuishi kwa hofu huku wakishindwa kufanya shughuli zao za kiuchuni hasa nyakati za jioni kwahiyo niliombe Jeshi la Polisi kufanya operesheni za mara kwa mara ili kukokemesha matukio kama haya" amesema

Ameongeza kuwa mbali na kufanya operesheni hizo kuwa endelevu lakini pia jeshi hilo linatakiwa kuwa na mahusiano mazuri na wananchi ili kuwarahisishia kazi zao ya kuwabaini wahalifu.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji cha Iramba, Matiko Ngelwacha amesema kuwa katika tukio lililotokea Septemba 20, 2022 kijini kwake jumla ya maduka matatu yalivamiwa ambapo mtu mmoja alijeruhiwa kwa kupigwa risasi huku zaidi ya Sh1 milioni zikiporwa na wahalifu hao.

"Tukio lilitokea kwenye saa 1.30 usiku na baadhi ya wahalifu tuliweza kuwatambua kwa sababu ilikuwa bado ni mapema.

“Siku moja baada ya tukio kuna watu walikamatwa na hii ni kutokana na ushirikiano uliotolewa na wananchi kwahiyo tunaomba doria zifanyike mara kwa mara ili tuishi kwa amani," amesema.

Kufuatia tukio hilo la mauaji ndugu wa marehemu wamegoma kuzika wakidai kuwa tukio hilo limegubikwa na sintofahamu na kutaka uchunguzi ufanyike.