Wananchi waeleza chanzo cha mafuriko Morogoro

Muktasari:

Baada ya Jeshi la Zimamoto na Uokoji kuokoa watu 48 wakiwemo watoto 39 kufuatilia nyumba zao kuzingirwa na maji kata ya Kihonda, baadhi ya wakazi  wamesema sababu ya nyumba zao kujaa maji ni uwepo wa miundombinu mibovu.



Morogoro. Baada ya Jeshi la Zimamoto na Uokoji kuokoa watu 48 wakiwemo watoto 39 kufuatia nyumba zao kuzingirwa na maji kata ya Kihonda, baadhi ya wakazi wamesema sababu ya nyumba zao kujaa maji ni uwepo wa miundombinu mibovu.

Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Januari 14, 2023 kuhusu mafuriko hayo yaliyotokana na mvua kubwa iliyonyesha juzi, wakazi hao wa kata ya Mambi, Mafisa na White House wamesema endapo miundombinu ya maji itajengwa vizuri na kusafisha mifereji kwa kuongeza kina, mvua kubwa ikinyesha athari haitakuwa kama ilivyo sasa.

Thekra Shiriri (77) amesema mtaa wao umekuwa ukikumbwa na mafuriko kwa sababu baadhi ya wananchi wamejenga katika njia za maji.

“Mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia jana imenyesha kwa saa tano, maji yakawa mengi na kukosa uelekeo na hii ni kutokana na mifereji kuzibwa kutokana na watu kujenga nyumba au ukuta katika njia za maji.” amesema Thekla.

Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa White House kata ya Mafisa, Saidi Njete amesema nyumba tano maji yameingia ndani na 10 zimezingirwa na maji  na hakuna mtu yeyote aliyepata madhara.