Wananchi waelimishwa kutumia nishati safi kuokoa miti Dar

Mwenyekiti wa bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA). Janet Mbene

Muktasari:

  • Tawen wamefunga semina ya kutoa elimu kwa wananchi inayohusu  matumizi ya nishati safi ili kunusuru miti pamoja na afya zao kwa Jiji la Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Wananchi wa Kigamboni wametakiwa kutumia fursa zinazotokana na nishati mbadala ili kujinusuru na changamoto za kiafya inayotokana na matumizi ya kuni na mkaa.

Hayo yameelezwa leo jumanne Septemba 12, 2023 jijini Dar es Salaam  na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Janet Mbene wakati wakifunga semina ya matumizi ya nishati safi iliyofanyika Wilaya ya Kigamboni.

Amesema wafanyabiashara wanaongoza kwa kutumia mkaa na kuni na hivyo kusababisha uharibifu wa mazingira na hata kupelekea kupata maradhi yatokanayo na moshi.

Amesema zipo tafiti ambazo zimefanyika zimeonyesha kuna baadhi ya wanawake wamepoteza ujauzito kutokana na matumizi ya kuni na hivyo wanaendelea kutoa elimu zaidi kwa wanawake.

"Watu wanapata changamoto za upumuaji kutokana na matumizi ya kuni ambayo yanaathiri mapafu yetu, watu wanapewa hadi lawama za mambo ya ushirikina kwa kuwa wana macho mekundu ambayo yamesababishwa na matumizi ya kuni," amesema Mbene.

Mbene amesema kwa sasa hamasa ya kuacha matumizi ya kuni na mkaa inaenda kutumika kwenye magereza ili kunusuru misitu ambayo inakatwa miti kwa wingi.

Pia amesema ili biashara ya kukata kuni na matumizi ya mkaa yafikie ukomo ni lazima watumiaji wabadilike kwa kuacha kutumia na wauzaji watakosa soko la wanunuaji.

"Wanawake wengi wanakwenda kutafuta kuni na wanapokutana na miti mibichi hawafikirii kwenye kukausha zaidi ya kupepea ili ikaukie kwenye jiko," amesema.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Tanzania Women Empowerment Network (Tawen), Florence Masunga amesema wameamua kusaidia wanawake katika masuala ya nishati safi ili kuwasaidia katika kuendeleza vipato vyao kutokana na biashara wanazofanya.

Pia, Masunga amesema kumekuwa na fikra potofu kwa baadhi ya watu kusema utumiaji wa gesi ni chanzo cha milipuko ndani ya nyumba na hivyo kupelekea wanawake katika baadhi ya maeneo kutotamani kutumia gesi.

"Tunafahamu kwa sasa wanawake wamejikita katika ujasiriamali ili kuendeleza familia zao ikiwepo biashara ya mama lishe na kujikuta wanatumia mkaa muda mrefu na wengine kupata maradhi mbalimbali yanayotokana na moshi," amesema Masunga.

Amesema muitikio wa wanawake katika kuachana na matumizi ya mkaa na kuni umekuwa mkubwa kutokana na hamasa inayotolewa na Serikali katika matumizi ya nishati mbadala hadi kufikia 2030 kusiwe na matumizi ya kuni na mkaa.

Mwakilishi wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Nishati, Anita Ringia amesema matumizi ya nishati safi yatamkomboa mwanamke ambaye muda mwingi anatumia mkaa na kuni.

"Tunafahamu kwenye utafutaji wa kuni kuna mambo mengi yanatokea ikiwepo ubakaji, utumiaji wa muda mrefu katika kutafuta kuni na hata baadhi ya watu kutokuwa na imani na watu wanoishi nao kwa kubadilika mwonekano halisi uliosababishwa na moshi,"amesema Ringia.

Amesema kwa sasa wanaendeleza yale yote yaliyopangwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati, Januari Makamba wakati akifungua semina ya matumizi ya nishati safi mwaka 2022.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Hc/Hq, Selina Letara amewataka wanawake kutumia fursa  zinazopatikana kwa ajili ya kujikwamua katika maendeleo na kufikia malengo waliojiwekea.

"Ukifuatilia historia za watu wengi humu kila mmoja ana njia zake ambazo alizitumia mpaka kufikia hapa hivyo kama tumeambiwa kuhusu mambo ya nishati mbadala ni muhimu kwa ajili ya afya zetu ni sehemu pekee za kuchota maarifa," amesema Letara.

Akielezea faida ya semina za nishati mjasiliamali Mtera Balele amesema Tawen wameona mateso wanayopata wajasiriamali kwa kutumia mkaa na kuni kwani wanapata fursa ya elimu kutoka kwa wafanyabiashara wa gesi na nishati mbadala.

"Nafanya biashara ya samaki na ninatumia kuni muda mwingi kwa kiasi fulani umeniathiri kifua hivyo kufika hapa na kupata elimu nakwenda kubadili matumizi ya nishati katika biashara yangu," amesema Balele.