Wananchi wafunguka mauaji ya mwanafunzi wakati akizikwa

Mwili wa Mwanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu Joseph,  Hajrat Shaban ukiwasili nyumbani kwao, Mtaa wa Kihonda-Kilimanjaro baada ya kutoka chumba cha kuhifadhia maiti Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro. Picha na Johnson James

Muktasari:

 Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Joseph, Julius Usiga amesema chuo kitamkumbuka Hajrat kwa upendo wake kwa wenzake na alikuwa kiunganishi kizuri kati ya uongozi wa chuo na wanafunzi

Morogoro.  Maziko ya mwanafunzi wa Chuo cha Mtakatifu Joseph aliyeuawa juzi kwa kuchomwa kisu na mtu asiyejulikana akiwa kwenye eneo la hosteli za chuo hicho, yamefanyika katika makaburi ya Kola, Morogoro.

Wakizungumza Leo Alhamisi Aprili 18, 2024 baada ya maziko hayo, baadhi ya waombolezaji wameliomba Jeshi la Polisi mkoani Morogoro  kuhakikisha linamtia mbaroni muuaji.

Hajrat Shaban aliuawa kwa kuchomwa na kisu mkononi na mgongoni  alipokuwa akiporwa simu yake ya mkononi.

Akizungumza msibani hapo leo, Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Joseph, Julius Usiga amesema chuo kitamkumbuka Hajrat kwa upendo wake kwa wenzake na alikuwa kiunganishi kizuri kati ya uongozi wa chuo na wanafunzi.

“Hivyo tunawaomba polisi wamsake muuaji ili sheria ichukue mkondo wake kwa sababu ametuondolea kijana wetu aliyekuwa hodari,” amesema.

Mwakilishi wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Richard Mkesi amesema kifo cha mwanafunzi huyo kimeligusa jeshi hilo.

“Wajibu mkubwa wa Jeshi la Polisi ni kulinda usalama wa raia na mali zao, kimsingi tumeguswa kwa sababu hapa kuna maisha ya mtu yamepotea na kuna mali za mtu zimepotea, hivyo tunao wajibu wa kuhakikisha wote walioshiriki katika tukio hili wanakamatwa na wanachukuliwa hatua kali za kisheria,” amesema Mkesi.

Amesema tangu tukio hilo litokee, polisi wanakesha kuwasaka wahusika na watahakikisha wanapatikana, hivyo amewataka wananchi wawe watulivu.

Mkesi amesema tukio hilo limewafungua macho na sasa wataongeza nguvu ya ulinzi katika maeneo hayo.

Hajrat anadaiwa kuuawa baada ya kuvamiwa akiwa hosteli za chuo hicho kilichopo Bwawani, Kata ya Mkundi.

Mwakilishi wa Benki ya CRDB, Juma Haji ambako Hajrat alikuwa akifanya mafunzo kwa  vitendo enzi za uhai wake amesema tangu aanze mafunzo alionesha bidii kwa kila kazi aliyokuwa akipangiwa kuifanya kila siku.

“Aliutumia muda wake wa ziada kufanya kazi hapa kwetu ya kujitolea na alikuwa mfanyakazi mzuri, hata siku mauti yanamkuta asubuhi yake mpaka mchana alikuwa mtaani akifanya kazi ya kuwafungulia akaunti wateja wetu,” amesema Haji.

“Tunamuomba Mungu ampokee na ampumzishe kwa amani.”

 Akizungumza msibani hapo, Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Kilosa, Gregory Nyansio alitoa wito kwa wananchi kuwafichua vijana wanaowatilia shaka kuwa ni wahalifu.

“Tusiwafuge huku mitaani, lakini wazazi tukemee matukio kama haya kwanza yanatia aibu na yanamaliza nguvu kazi ya Taifa,” amesema Nyansio.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa chuo hicho, Amos Dimata amesema mauaji ya Hajrat yameacha fumbo kwa wanafunzi wote.

Hata hivyo, ameliomba Jeshi la Polisi kudhibiti matukio ya kihalifu yanayotokea mara kwa.

“Matukio ya kihalifu ni mengi katika Mtaa wa Bwawani na yanatishia sana usalama wetu sisi wanafunzi, tunaporwa sana mali zetu na sasa wamefikia hata kupoka uhai wetu, tunawaomba polisi walitazame kwa jicho pana zaidi eneo hili,” amesema Dimata.

Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Twaha Kilango amesema kuna haja kwa polisi kupandikiza wachunguzi kila mahali kwa sababu hali ya usalama mkoani humo inazidi kuzorota.

“Hali ya usalama kwenye mkoa huu imekuwa tete, baadhi ya vijana wa bodaboda wamekuwa hatari, ona sasa wamekatisha maisha ya binti huyu Hajrat Shaban na sasa hayupo tena, mji huu matukio kama haya yanajirudiarudia kila wakati, nadhani umefika wakati Serikali kuchukua hatua, mtu hawezi kutembea na simu barabarani anakwapuliwa, hali ni mbaya, polisi mnakazi ya kufanya tena kubwa,” amesema Sheikh Kilango.