Wananchi waipa ‘tano’ Serikali – Ripoti
Muktasari:
- Matokeo ya utafiti wa maoni ya watu uliofanywa na Repoa unaonyesha Watanzania wanaridhishwa na ushiriki wa wanawake katika fursa mbalimbali
Dar es Salaam. Asilimia 82 ya Watanzania wanaridhishwa na jitihada zinazofanywa na Serikali kuweka kukuza usawa na fursa za kiuchumi kwa wanawake.
Hiyo ni kwa mujibu wa utafiti wa Afrobarometer uliofanywa na Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa), ilijikita katika maeneo matano yakiwemo uchumi, utawala wa sheria, demokrasia na uaminifu kwa taasisi za umma.
Utafiti huo unaonyesha pia asilimia 61 wanafurahia utawala mzima wa uchumi wa nchi, lakini wanajali zaidi kupanda kwa bei na ajira kwa vijana.
Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari amesema asilimia 82 ya waliohojiwa wanaridhishwa na kiwango kikubwa cha kushughulikia mahitaji ya elimu huku asilimia 69 ya wananchi wakiridhishwa na utoaji wa huduma za msingi za afya kutoka serikalini.
“Kwa ujumla haya ni maoni ya wananchi juu ya eneo la uchumi, pamoja na kwamba wameona kuna changamoto ya mfumuko wa bei na ajira, lakini bado wana imani na Serikali yao kuwa inaendelea kufanya vizuri, hii ina maana kwamba wananchi wanatoa mwelekeo wa maeneo ambayo taasisi za umma zinatakiwa kufanyia kazi,” amesema.
Kwa upande wa demokrasia waliohojiwa kuhusu hali ya hewa walisema ingawa kukiwa na changamoto za hapa na pale wananchi wanafurahishwa na jinsi demokrasia inavyofanya kazi nchini.
Akizungumzia matokeo hayo mtafiti wa masuala ya jinsia Loreen Kiswaga amesema utafiti huo ni mzuri, umeonyesha jinsi wanawake wameweza kushirikishwa katika ngazi mbalimbali za maamuzi, pamoja na jinsi wananchi wanavyoridhishwa na maendeleo ya nchi, ambayo ni maendeleo makubwa ikilinganishwa na miaka ya nyuma ya ushiriki wa wanawake katika ngazi za kufanya maamuzi ulikuwa mdogo.