Wananchi wamjia juu mbunge anayesema posho, mishahara yao haitoishi

Wananchi wamjia juu mbunge anayesema posho, mishahara yao haitoishi

Muktasari:

  • Siku mbili baada ya  mbunge wa Mbogwe (CCM), Nicodamus Maganga kusema mshahara na posho za mbunge hazitoshi, watu wa kada mbalimbali wamemjia juu.

Dar es Salaam. Siku mbili baada ya  mbunge wa Mbogwe (CCM), Nicodamus Maganga kusema mshahara na posho za mbunge hazitoshi, watu wa kada mbalimbali wamemjia juu.

Wakitoa maoni yao katika mtandao wa kijamii wa Instagram wa Mwananchi  ulioweka habari hiyo na video ya mbunge huyo akieleza hali ngumu ya wabunge, baadhi ya watu hao wamemtaka mbunge huyo kuachana na kazi hiyo ya uwakilishi wa wananchi kama anaona haina maslahi.

Maganga aliyasema hayo Jumatatu Juni 21, 2021 bungeni mjini Dodoma wakati akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22, akiwataka wabunge wenzake kuwaambia ukweli wananchi.

 “Kama hazitoshi ajiuzulu ubunge arudi kwenye kazi yake ya awali,” ameamdika Langoon_Sanmorino.

Kauli hiyo imeungwa mkono na Tairo.Florianofficial akisema, “kawaida pesa haijawahi kutosha...,kwenu ndugu wananchi.”

Naye Emanuelyjaphet6790 amesema kauli hiyo ni dalili la ombwe la wabunge wa upinzani bungeni, “bila shaka tutajua umuhimu wa upinzani inawezekana tulikuwa hatuelewi hivi mtu analipwa milioni 12 na bado hazitoshi na mwalimu anayelipwa 400,000 asemeje? Du! Ama kweli.”

Wakati Jk_shoot_it akidai kuwa mshahara wa mbunge ni sawa na mtaji wa kijana mtaani, Nasra7162 amesema,“ndio tabu yakuchagua wabunge masikini, njaa ndio zinawapeleka bungeni wapo kuwaza mishahara na sio kutatua shida za wananchi waliowapigia kura.”

Shab652 amesema, “sasa si muache mje huku kuwa wajasiriamali? Tena ningekuwa naweza kushauri Bunge lisiwe na wabunge zaidi 100, maana ukiangalia sana wabunge wenye michango ya maana yenye kuisaidia nchi hawafiki hata 50.”

“Wataalam wanaacha taaluma na wengine walikuwa waalimu vyuo vikuu wamekimbilia bungeni, wengine wanatumia nguvu kubwa kushinda ikiwepo rushwa mshaingia bungeni mnasema maslahi madogo mnatuonaje kwani?”

Naye Bakari_Kaisi amehoji kuhusu mijadala ya wabunge akilinganisha na posho na mishahara.

“Walipoomba kura walikuwa wanasema tunawatuma wala hawaendi kufuata pesa, walisema wanakwenda kuleta haki na maendeleo. Sasa posho mishahara. Hivi wanajua huku uraiani watu wanaishi maisha gani,” amehoji.