Wananchi wamtaka mbunge kunywa maji ‘machafu’

Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi akiwa ameshika chupa yenye maji aliyopewa anywe na wakazi wa mtaa wa Mtemibeda kata ya Misunkumilo. Picha na Mary Clemence.

Muktasari:

  • Wananchi wa mitaa ya Milupwa na Mtemibeda mjini Mpanda wamtaka mbunge wao kunywa maji yasiyo salama mithili wanavyokunywa wao lengo atatue changamoto hiyo.

Katavi. Wakazi wa mitaa ya Milupwa na Misunkumilo Manispaa ya Mpanda wamelalamikia changamoto ya ukosefu wa maji ambapo inawalazimu kutumia maji yasiyo safi na salama.

 Mbele ya Mbunge wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi leo Augosti 4, 2023 wakazi hao wamesema eneo hilo halina bomba hata moja wanatembea umbali mrefu kwenda kuchota maji machafu.

"Kupitia wimbo wakiwa wamebeba chupa ya plastiki iliyo na maji yasiyo salama walimuomba kunywa maji hayo ishara ya kutatuliwa kero hiyo," amesema.

"Walisikika kwa sauti moja tunaomba unywe pombe hii uone ilivyo tamu," zilisikika sauti zao.

Joyce John mwananchi wa eneo hilo, amesema maji hayo yanawaathiri kiafya kwa kuwa wamekuwa wakiugua matumbo ya kuhara mara kwa mara na watoto wao.

"Tumekuja nayo makusudi anywe maana tunafahamu hawezi kunywa anaogopa, atusaidie kuisimamia serikali itatue changamoto hii," amesema Joyce.

Diwani wa Kata ya Misunkumilo Matondo Kanyigu akagongela msumari suala hilo akidai litatufutiwe mwarobaini ili kunusuru hali hiyo.

“Mbali na changamoto hizo pia wanakabiliwa na changamoto ya barabara na nishati ya umeme, vitu hivi tukivipata wakazi hawa wataendelea kuwa na raha,” amesema.

“Watakuwa na imani na serikali yao inayoongozwa na Chama Cha Mapinduzi, Mbunge barabara ya kutoka Misunkumilo-Utemini kuelekea misheni, wananchi wanahoji ni lini itakamilika,” amesema Kanyigu.

Aidha Kapufi kabla ya kutolea majibu kero hizo akahitaji kupata ufafanuzi kuhusu ukosefu wa maji kutoka ofisi ya Mamlaka ya Majisafi mjini Mpanda (Muwasa).

“Yupo mwakilishi hapa naomba uwaeleze wananchi hii kero itapatiwa ufumbuzi lini ili wananchi waondokane na tatizo hilo?” ameeleza.

Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi mjini Mpanda, Rehema Nelson akataja mikakati miwili ya muda mfupi na mrefu ili kukabiliana na changamoto ya maji.

“Nimesikitika kuona yale maji mliyompa mbunge wenu, mmesema mnayatumia kunywa, mkakati wetu wa kwanza tumeona kuna uhitaji wa kuwachimbia kisima wakati mkakati wa muda mrefu ukiendelea,” amesema.

Ameongeza kuwa mkakati wa muda mrefu ni wa kusambaza  maji kutoka bwawa la Milala ambapo hadi sasa mkandarasi yupo eneo la mradi anaendelea kufanya usanifu na unatarajiwa kukamilika Oktoba 2025.

“Kwa huu muda mfupi tutamtuma meneja ufundi aje aangalie hili eneo na litafanyiwa utafiti, tutawachimbia kisima mpate maji safi,” amesema Rehema.

Hatimaye Mbunge Kapufi akawaondolea wasiwasi wananchi kuwa Serikali inatambua kilio chao na imeanza kutekeleza mradi mkubwa wa maji katika miji 28 nchini.

“Mpanda tumepata bahati ya kusambaziwa maji kilometa 42 ni nyingi ikilinganishwa na maeneo mengine, pia kuna mpango mkakati wa kuleta maji kutoka Ziwa Tanganyika,” amesema Kapufi.

Changamoto ya barabara amewaomba wananchi kutoa ushirikiano ili waletewe greda la kutengeneza yeye yupo tayari kuchangia jitihada zao.

“Mapinduzi wananchi walichangia nikawaongezea, wananchi wa Shanwe nao wamesema tayari wana shilingi milioni moja na laki tano greda linagombaniwa,” amesema.

Amesema halmashauri kupitia bajeti ijayo imekusudia kutenga Sh100 milioni kwa ajili ya kuchonga barabara.

“Tarura nao awamu hii wameongezewa fedha za kutosha kwaajili ya maboresho ya barabara, natumia fursa hii kumshukuru sana rais wetu,” amesema.