Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wananchi wamvamia mwekezaji mgodini

Muktasari:

  • Mgodi wa Dirif wasitishwa kutoa huduma baada ya wananchi kumvamia mwekezaji aliyeletwa na kikundi cha Kagera wakishinikiza aondoke kwa kuwa ni mali ya wananchi.

Katavi. Mgodi wa Kijiji cha Dirif uliopo Manispaa ya Mpanda umesitishwa kutoa huduma na Serikali kutokana na taharuki iliyotokea baina ya wananchi na wasimamizi wa mgodi huo kikundi cha Kagera wanaolalamikiwa kuleta mwekezaji kinyemela pasipo kuwashirikisha kwa lengo la kujinufaisha wenyewe tofauti na taratibu walizojiwekea.

 Taharuki hiyo imedumu zaidi ya masaa 11 kuanzia asubuhi hadi jioni Mei 5, 2023 baada ya wananchi wa Kijiji cha Dirif kuuvamia mgodi huo  wakimtaka Mwekezaji Kamtoni, kusitisha shughuli za uchimbaji dhahabu kwa kuwa eneo hilo lina mgogoro muda mrefu na linamilikiwa na wananchi.

Wakazi hao  walisikika wakipaza sauti zao “tunataka mlima wetu” wakidai hawana imani na uongozi wa kikundi cha Kagera waliowapa dhamana ya kusimamia mgodi huo kisha kutafuta leseni ya umiliki wao binafsi.

Mussa Keta mkazi wa kijiji hicho amesema mgogoro baina yao na kikundi hicho ulianza 2022 hadi sasa na kwamba walishatoa taarifa ofisi ya Mkuu wa wilaya ya Mpanda lakini imeshindwa kuutatua.

“Tunashangaa ofisi imeshindwa kutoa maamuzi kwasababu leseni inayotumiwa na kikundi cha Kagera ni ya wananchi wote, viongozi walikuwa wanapeleka dhahabu soko la madini tumewachoka kwa ufisadi wao,” amesema.

“Hadi sasa tunawadai zaidi ya Sh45 milioni, tunachoshangaa wanaleta mwekezaji bila wananchi kujua, tumeona grenda linakwangua ndo maana vurugu zimetokea, kwa mwezi wanakusanya Sh4 milioni zinakwenda wapi?” amesema.

Amesema matarajio yao fedha hizo zitumike kuboresha miundombinu ya shule na miingineyo lakini hadi sasa shule yao haina choo cha walimu na huduma ya maji  hali iliyopelekea  mradi ujenzi wa zahanati kukwama.

“Kuna watu wengi wakiwamo wazee na vijana wanategemea kunufaika na mgodi huu lakini hawanufaiki na chochote wanaonufaika ni watu nane pekee hatuwataki tuliwachagua sisi sasa wametosha kutuibia,” amesema.

“Unaona risasi hizi zimepigwa baada ya wananchi kumfuata mwekezaji kumushusha pale, askari aliyeletwa kuwalinda akafyatua, anapiga wachimbaji wanaotafuta ridhiki, hizi zinatakiwa kupigia majambazi, watu walipata hasira wakarusha mawe,” amesema Keta.

Kilio cha wananchi hao wanahitaji ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Katavi kuingilia sakata hilo kwa madai kuwa, hawamtaki mkuu wa wilaya kwasababu anauchochea mgogoro huo na kupelekea kukosa haki yao ya  kupata mahitaji na kusomesha watoto.

Imedaiwa kuwa baada ya mgogoro huo kuwasilishwa Ofisi ya Mkuu Wilaya ya Mpanda alikwenda Kaimu Mkuu Wilaya, Onesmo Buswelu akaelezwa changamoto hiyo na wananchi kupitia mkutano wa hadhara.

“Aliuliza huu mgodi ni wa kikundi cha Kagera au wananchi? mmoja wa kiongozi kutoka kikundi hicho alijibu ni wa wananchi, akauliza mnataka nini tukajibu uongozi uliopo utoke tuchague wapya na mwekezaji Kamtoni hatumtaki,” amesema.

“Wakakubali wakasema hatuwezi kutoa majibu sasa hivi tutaenda kukaa kikao tujadili tulete mwafaka, kabla ya pasaka tulitakiwa kupewa taarifa lakini hatujapata na kazi zinaendelea,”amesema Lwiza Nkomedi.

Aidha amesema majibu wanayopata kutoka kwenye kikundi cha Kagera ni kwamba wameidhinishwa na ofisi ya mkuu wilaya, mgodi ni mali yao bila maandishi au kuitisha mkutano wowote kama walivyoahidiwa.

Mkazi mwingine wa kijiji hicho Hamisa Masebu amesema baada ya eneo hilo kugundulika kuwa lina madini aina ya dhahabu wananchi walitozwa fedha kulingana na uwezo wao.

“Mimi nina mgahawa nilitozwa sh5000 wengine Sh100,000 na kuendelea, tukawachagua viongozi wasimamie lakini wanajinufaisha wenyewe tunamuomba Rais (Samia Suluhu Hassan) atusaidie,  eneo hili halina mashamba tunategemea mgodi huu,”Hamisa.

Mmoja wa wanakikundi cha Kagera Emmanuel Masumbuko amesema mgodi huo ni mali yao baada ya kujiunga kwenye kikundi cha watu 28 walifuata taratibu zote wakakata leseni kisha kutafuta mwekezaji.

“Tulifika ofisi ya usajili na madini tukapata leseni na nyaraka zote, huu ni mwaka wa saba tunafanya shughuli zetu kwa ushirikiano mzuri na wananchi tumebaki wanachama 20 wengine walikufa na baadhi walijitoa,” amesema.

 “Tatizo lilianza tulipoanza kuuza makinikia, tumeuza mara mbili michango  ya kijiji tunachangia, walikuja viongozi wawili Diwani na Afisa Mtendaji wa kata wakaomba wajiunge na kikundi chetu tukakataa kwasababu wao ni watumishi wa  serikali,” amesema Masumbuko.

Amesema viongozi hao walihisi makinikia yana fedha nyingi, walivyowakatalia walitamka wazi lazima tuwanyang’anye leseni, wakaamua kupiga kampeni za chinichini kuwashinikiza wananchi hao kufanya vurugu hizo.

Baada ya wananchi hao kuwavamia waliwashambulia kwa mawe na marungu huku wakiponda grenda la mwekezaji kwa mawe na kusababisha uharibifu mkubwa.

“Tulikimbia wanakikundi wote baadhi wamejeruhiwa akiwemo askari wetu, serikali ilishatuamuru kuendelea kuchimba cha kusikitisha tumevamiwa tunasubiri  mamlaka ije itusaidie,” amesema.

Kwa upande wake Diwani wa kata ya Magamba Fortunatus Chiwanga anakiri kupokea malalamiko ya wananchi wa Dirif kuhusu mgogoro baina yao na kikundi cha Kagera akidai aliufikisha ofisi ya kata kupitia kikao cha WODC.

“Tulijadiliana tukawaandikia barua kikundi cha Kagera wakakubali kuwa huo mgodi ni mali ya wananchi baadaye walikataa,nikaupeleka ofisi ya CCM wilaya,” amesema.

“Ofisi ya CCM wilaya ikaiagiza ofisi ya mkuu wilaya kuutatua, lakini haikufanyi hivyo nashangaa juzi napigiwa simu kuna vifaa vimeletwa kuchimba bila wananchi kushirikishwa,” amesema.

Ameongeza kuwa kutokana na vurugu zilizojitokeza ni dhahiri kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya iliyofika eneo hilo kushuhudia imejiridhisha kwamba mgogoro huo haujaisha.

“Imeonekana wazi pamoja na kikao kile kufanyika lakini bado hali ni mbaya, ninawaomba wananchi muache uvunjifu wa amani waache watatufute suluhu siyo kutembea kwenye magari tu,”amesema Chiwanga.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Mpanda, Sophia Kumbuli aliyeambatana na kamati ya ulinzi na usalama amesitisha huduma katika mgodi huo, akiwaomba wananchi kuwa na subira hadi suluhu itakapopatikana.

“Hatutaki kuona tone la damu linamwagika, kwasababu tutaweka doa Tanzania, Katavi ,Mpanda, Magamba hadi Dirif yetu,amani yetu inayoimbwa na kuonewa wivu na nchi za nje lazima tuilinde,” amesema.

“Vitu vingi vinaishia mezani hata ndani ya ndoa mkikorofishana mnamalizia mezani, kwanini mgombane hivyo tumekuja kuliona hili ni kweli kuna gepu lakini tunakwenda kumalizia tutaleta majibu, amani iwepo,”amesema Kumbuli.

Kijiji cha Dirif kilichopo Kata ya Magamba Manispaa ya Mpanda kinazungukwa na milima inayosadikika kuwa na madini ya dhahabu ambapo wananchi wake wanategemea zaidi shughuli za uchimbaji  kujitafutia kipato.