Wananchi wanaodai fidia wasusia mkutano wa RC Katavi

Graison Katikile, mwakilishi wa wananchi wanaodai fidia akieleza hatua waliyofikia akiwa ni miongoni mwa mwa wananchi waliosusia kikao cha mkuu wa mkoa wa Katavi. Picha na Mary Clemence

Muktasari:

  • Wananchi wanaodai fidia ya kupisha mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji bwawa la Milala mkoani Katavi wamesusia mkutano wa mkuu wa mkoa Katavi kwa madai majibu yake hayaridhishi.

Katavi. Wananchi wanaosubiri fidia kupisha mradi wa ujenzi wa chanzo cha maji bwawa la Milala, Manispaa ya Mpanda, wamesusia kikao cha Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko kwa madai kuwa majibu katika mikutano yake mitano iliyopita hayaridhishi.

 Wananchi hao kutoka kaya zaidi ya 500 katika Kata ya Shanwe na Misunkumilo, wamejenga ndani ya hifadhi ya chanzo cha maji bwawa la Milala kwa madai kuwa waliuziwa na Serikali.

Kupitia ziara ya mawaziri wanane kujiridhisha na kutoa mapendekezo kwenye maeneo yenye migogoro ya ardhi, waliamuru wananchi hao walipwe fidia kwa kuwa hawakuvamia isipokuwa wameuziwa.

Kutokana na hali hiyo, wananchi waliridhia kusubiri fidia ili wapate fedha za kununua viwanja  sehemu nyingine na kujenga makazi.

Kilio cha wananchi hao ambacho wanakitoa mara kwa mara kwa viongozi wa chama tawala na Serikali ni ucheleweshwaji wa malipo ya fidia.

Leo Februari 20, 2024 Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko ameitisha mkutano, ili kusikiliza kero kwa wananchi hao, lakini hawakufika.

Wananchi hao wameeleza kuwa wamesusa kikao hicho kwa sababu suala hilo lilipofikishwa kwa kiongozi huyo alidai atafuatilia, lakini hakuna ufuatiliaji na majibu yake yamekuwa yakifanana.

“Leo anajibu anafuatilia hadi lini? Watu nyumba zetu zimebomoka na tumeshathaminishwa, siku 90 zimepita sheria inasemaje?

“Wengine wana watoto wanasoma wameshindwa kwenda shule kwa sababu ya miundombinu mibovu, analotamka leo ndiyo yale yale yanasemwa kwenye vikao,” amesema Graison Katikile.

Kwa upande wake, Mponeja Bahebe, mkazi wa Shanwe amesema wamefanyiwa tathmini muda mrefu, lakini wakiuliza utekelezaji wake, hawapati majibu ya kuridhisha.

 “Mkuu wa mkoa kila siku anasema linashughulikiwa, chumba kimoja tunaishi watu saba, tumekatazwa kujenga na kulima, tunaomba watulipe tukajenge nyumba bora, vifaa vinapanda bei.

 “Mimi nadai Sh2 milioni, wanavyochelewesha fedha tutashindwa kuitumia tunavyotegemea, idara ya maji inayohusika iseme kama imeshindwa tuendelee kujenga,” amesema Bahebe.

Wameongeza kuwa waliposikia kuna kikao hicho walipata matumaini ya kupata majibu kwamba watalipwa fidia zao,       lakini majibu yamejirudia.

Akizungumzia malalamiko hayo, mkuu wa mkoa Mwanamvua Mrindoko amekiri tathmini hiyo kufanyika kupitia Wizara ya Maji na kwamba wameshapeleka majedwali kupitia ofisi ya katibu tawala mkoa.

“Taratibu za kulipwa fidia tunasubiri wizara tunaendelea kufuatilia, kama waziri ananisikia naomba wananchi wa Milala walipwe wametii kupisha mradi,” amesema Mrindoko.