Wananchi wapongeza upigaji kura Mbarali

Karani anayeongoza wapiga kura akimuonyesha majina moja wa wananchi waliofika kupiga kura.

Muktasari:

  • Leo Jumanne Septemba 19 wananchi baadhi ya wananchi wa Mbarali mkoani Mbeya wamejitokeza kupiga kura ya kumchagua mbunge atakayeziba nafasi iliyoachwa wazi na Francis Mtega aliyefariki dunia Julai Mosi.

Mbarali. Baadhi ya wananchi wa Mbarali waliojitokeza kupiga kura kumchagua mbunge wa jimbo hilo mchakato huo unakwenda vizuri na wasimamizi wanaowaongoza vyema na wanachosubiri matokeo ya mshindi.

 Wameyasema hayo leo Jumanne Septemba 19, 2023 wakati walipojitokeza kupiga kura katika vituo mbalimbali vilivyopangwa kwa ajili hiyo ili kumpata mbunge atakayeziba nafasi iliyoachwa na Francis Mtega aliyefariki dunia Julai Mosi mwaka huu kwa kugongwa na trekta shambani kwake.

Jimmy Nyagawa aliyepiga kura katika Kituo cha Shule ya Msingi Ubaruku amesema makarani waliopangwa wanatoa ushirikiano vizuri akisema ikitokea mtu hajui kusoma na kuandika anapewa usaidizi wa kufanikisha kutumia haki ya msingi kupiga kura.

"Naomba waliopo nyumbani wajitokeze kwa wingi kupiga kura kwa sababu ni haki yao ya msingi, waje tufanye uamuzi sahihi, hadi muda mchakato unakwenda vyema," amesema Nyagawa.

Natheliian Kashu amesema mchakato unakwenda vizuri lakini baadhi ya wananchi hawaoni majina yao inawalazimu kufuatilia kwa wahusika, ingawa siyo kazi rahisi kupata jina lako kama halipo kwenye karatasi zilizobandikwa ukutani.

Naye Kibibi Mjengwa amesema alifika saa 2 kamili katika kituo akisema aliahaingika huku na kule kutafuta jina lake, lakini mwisho wa siku alifanikia kulipa na kupiga kura. Amewataka waliokosa majina nje wafuatilie ndani watayapata.

"Pia wanaosimamia mchakato huu wawe wepesi kuwapa ushirikiano wananchi wa kuangalia majina yao ndani endapo nje yakikosekana," amesema Kibibi.

Mpigakura mwingine Joyce Mtemelwa amesema hali ni shwari na alitafuta jina lake dirisha la kwanza hakuliona lakini alipoelekezwa sehemu nyingine ndani ya kituo hicho aliliona na kupiga kura.

Bruno Bugumba ambaye ni msimamizi wa kituo namba tatu Shule ya Msingi Ubaruku amesema walifungua kituo saa moja asubuhi na wananchi wameendelea kujitokeza kadiri muda unavyozidi kwenda wanajitokeza zaidi na utulivu upo.

Kuhusu wanaokosa majina, Bugumba amesema,  "Hapa shule ya msingi kuna vituo vinne, akikosa kituo kimoja anaelekezwa kwenye kituo kingine kulingana na majina yalivyopangwa na herufi.

"Utakuta mtu amekuja kituo fulani kumbe kina lake lipo kitu kingine basi tunamwelekeza huko anakwenda. Vivyo hivyo wenzetu wakikumta mtu hajaliona jina lake wanamwelekeza kituo kingine," amesema Bugumba.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), vyama vinavyoshiriki uchaguzi huo ni 13 vya CCM, ACT- Wazalendo, AAFP, DP, UNDP, UMD, UPDP, Ada- Tadea , NLD, CCK, TLP, Demokrasia Makini na ADC.