Wananchi watakiwa kutumia ‘birthday’ zao kupanda miti
Muktasari:
- Viongozi wa dini nchini wameshauriwa kuwahamasisha wananchi kutumia siku za kumbukumbu zao za kuzaliwa (birthday ) kupanda miti katika maeneo mbalimbali yanayowazunguka, kama sehemu ya zawadi zao za kukumbuka siku hiyo.
Arusha. Viongozi wa dini nchini wameshauriwa kuwahamasisha wananchi kutumia siku za kumbukumbu zao za kuzaliwa (birthday ) kupanda miti katika maeneo mbalimbali yanayowazunguka, kama sehemu ya zawadi zao za kukumbuka siku hiyo.
Mbali na kumbukumbu ya kuzaliwa, pia wametakiwa kutumia siku za kumbukumbu zao za ndoa na kipaimara kupanda miti, hatua ambayo itachochea ari ya utunzaji mazingira na kudhibiti ukataji miti ovyo.
Hayo yamesemwa leo Novemba 9, 2023, wakati wakipewa mafunzo ya athari za mabadiliko ya tabia nchi yaliyokuwa yakitolewa na shirika la Kilimanjaro Consortium for Development and Environment (KCDE) kwa kushirikina na Konrad Adenauer Stiftung (KAS) lengo likiwa ni kukabiliana na athari za mazingira ambazo zinaitesa dunia kwa sasa.
Akitoa mafunzo hayo kwa viongozi wa dini kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara, balozi wa mazingira nchini, Padri Profesa Aidan Msafiri, amesema viongozi wa dini wanaaminiwa na waumiwa hivyo wakitumia nafasi yao vyema swala la uharibifu wa mazingira litaweza kuthibitiwa kwa kiasi kikubwa.
Amesema katika kumbukizi za kuzaliwa, watu wamekuwa wakipewa zawadi za maua, fedha, keki na nyingine hivyo ni vyema wakajenga utamaduni wa kupanda miti kama sehemu ya zawadi hizo na kuitunza ili kuweza kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
"Viongozi wa dini mnaaminika kuliko watu wengine katika jamii hivyo mkitumia nafasi zenu kuna uwezekano makubwa wa kurejesha uoto wa asili na kuondokana na makali ya mabadiliko ya tabia nchi ambayo kwa sasa yanatikisa dunia," amesema
Profesa Aidan Msafiri, amesema ipo haja ya viongozi wa dini, kuanzisha klabu za mazingira na kuzishindanisha ili waumini wewe na ari ya kupanda miti hatua ambayo italeta mabadiliko.
Balozi huyo amesema, kuna haja ya kuwepo kwa utaratibu wa kutumia matamasha makubwa yanayofanyika hapa nchini, kutenga siku ya kupanda miti kabla ya kufanyika tukio husika.
Msaidizi wa Askofu Dayosisi ya Mwanga, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Mchungaji Timothy Jonas amesema mafunzo hayo yamewapa mwanga viongozi wa dini na kupata, mbinu mpya za kuhamasisha waumini kupanda miti.
Amesema suala la kuanzisha vilabu vya mazingira ndio jambo ambalo litaenda kuleta mafinikio chanya ya kukabiliana na uharibifu wa mazingira.
Meneja Miradi Shirika la Konrad Adenauer stiftung (KAS), Damas Nderumaki amesema shirika limekuwa likiwezesha viongozi wa dini mbinu za kuhamasisha waumini kupanda miti, pamoja na kuitunza ili kuondokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Amesema mafunzo hayo yametolewa kwa viongozi wa dini mbalimbali 30 kutoka mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.