Wananchi ‘wavurugwa’ mvua ya mawe yaharibu tumbaku ekari 90
Muktasari:
- Mvua ya mawe yaharibu ekari 90 za Tumbaku na kusababisha hasara kwa Wakulima 35, DC ataka vyama vya ushirika kuwa na mfuko wa maafa utakaowasaidia wakulima wakipata majanga.
Chunya. Ekari 90 za zao la tumbaku zimeharibiwa na mvua zinazoendelea katika Kata ya Lupa na Mtande wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya ambapo zaidi ya wakulima 30 wameathirika.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Mayeka Mayeka amewatembelea wakulima hao na kuwakumbusha kuwa umuhimu wa kukata bima ya mazao ili iweze kuwasaidia kupata fidia pindi wanapopata majanga.
Mayeka pia amewataka viongozi wa Vyama vya Ushirika vya Tumbaku kuweka mfuko wa maafa kwa wakulima wa zao hilo ili yanapotokea mambo kama hayo, mfuko utumike kumsaidia mkulima ambaye atapata majanga.
“Natoa pole kwa wakulima kutoka vyama vya Ushirika vya Lupatingatinga na Mtande kwa madhara haya ya mazao yenu kuharibiwa na mvua kubwa iliyonyesha,”amesema Mayeka.
Akizungumza na mwananchi mmoja wa wakulima waliothiriwa na mvua hizo, Elisha Bahati amesema mvua imeharibu tumbaku kipindi ambacho ni msimu wa kuchuma na kuziandaa kwa ajili ya kwenda sokoni hivyo kwa mwaka huu wao wanahesabu wamepata hasara.
Ofisa Kilimo Wilaya ya Chunya, Cuthbert Mwinuka amesema wanaendelea kufanya tathmini ya uharibifu wa mvua mazao katika wilaya nzima na itakamilika itatolewa.