Wanandoa kortini kwa kusafirisha heroin

Mkazi wa Mwembechai, Mwinyi Chande mwenye shati la bluu pamoja na mkewe, Halima Zahoro wakitoka kwenye chumba cha Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo Ijumaa Mei 19, 2023 jijini Dar es Salaam. Picha na Pamela Chilongola

Muktasari:

  • Mwinyi Chande (50) pamoja na mkewe Halima Zahoro (39) wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 21.21.

Dar es Salaam. Mkazi wa Mwembechai Mwinyi Chande (50) pamoja na mkewe Halima Zahoro (39), wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 21.21.

 Hata hivyo Wakili wa Serikali aliyetambulika kwa jina moja, Panklasia aliyekuwa anaendesha shauri hilo alimweleza mwandishi wa gazeti hili kuwa haina haja ya kuandika taarifa ya kesi hiyo.

"Haina haja ya kujua jina langu siyo lazima ndugu mwandishi uandike hii taarifa halafu siyo lazima nikutajie jina langu kama mawakili wengine wanakutajia majina yao ni wao siyo mimi," alidai Panklasia.

Wakili Panklasia akisoma hati ya mashtaka leo Mei 19, 2023 mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Francis Mhina alidai Machi 31, 2023 maeneo ya Magomeni walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa gramu 21.21.

Alidai upelelezi wa shauri hilo umekamilka hata hivyo washtakiwa hao walikana makosa yanayowakabili.

Hakimu Mhina alisema dhamana ipo wazi kwa washtakiwa hao kila mmoja anatakiwa awe na fedha taslimu kiasi cha Sh10 milioni au hati yenye thamani ya kiasi hicho pamoja na mdhamini mmoja.

Hata hivyo washtakiwa hao wamerudishwa rumade baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.