Watatu kortini usafirishaji heroin kilo 58.62
Muktasari:
- Watu watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na kosa la kusafirisha dawa za kulevya kilo 58.62 aina ya heroin.
Dar es Salaam. Wafanyabiashara watatu, wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na shtaka la kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo 58.62.
Washtakiwa hao ni Goodness Remy mkazi wa Salasala, Emmanuel Chigbo Mkazi wa Goba na Paulina Mwanga, mkazi wa Kibaha.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi ya uhujumi uchumi ambao walisomewa mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Amir Msumi.
Wakili wa Serikali Frank Michael, alidai washtakiwa hao walitenda kosa hilo Aprili 19, 2023 eneo la Salasala, wilaya ya Kinondoni jijinin Dar es Salaam.
Alidai washtakiwa hao wakiwa eneo hilo walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroin zenye uzito wa kilo 58.62.
Michael alidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na aliiomba Mahakama hiyo ipange tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu aliwaeleza washitakiwa hao kuwa, mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi yao na kwamba shtaka linalowakabili halina dhamana hivyo watapelekwa mahabusu hadi Juni Mosi, 2023 litakapokuja kwa ajili ya kutajwa.