Wanaochelewa kulipa kodi ya pango la ardhi kupewa nafuu

  • Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023, jijini Dodoma leo. Mabula ameliomba bunge lipitishe bajeti ya wizara yake kiasi cha Sh110.3 bilioni. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inakusudia kufanya marekebisho ya Sheria ya Ardhi ili riba ya kuchelewa kulipa kodi ya pango la ardhi ianze kutozwa baada ya kuisha kwa mwaka wa fedha badala ya miezi sita.

Dodoma. Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi inakusudia kufanya marekebisho ya Sheria ya Ardhi ili riba ya kuchelewa kulipa kodi ya pango la ardhi ianze kutozwa baada ya kuisha kwa mwaka wa fedha badala ya miezi sita.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dk Angela Mabula wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Amesema Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 imeweka utaratibu wa kukadiria, kutoza, muda wa kulipa na hatua za kuchukuliwa kwa mmiliki atakayeshindwa kulipa kodi hiyo kwa wakati.

Amesema kwa mujibu wa Kifungu cha 33(1) cha Sheria hii, mmiliki wa ardhi anatakiwa kulipa kodi ya pango la ardhi kwa mwaka kama ilivyoainishwa chini ya masharti ya Sheria ya Fedha za Umma.

“Kwa muda mrefu kumekuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi yanayotokana na takwa la kisheria la kutoza riba baada ya miezi sita ndani ya mwaka wa fedha ambao kodi ya pango la ardhi inapaswa kulipwa,” amesema.

Amesema ili kuondoa malalamiko hayo, Wizara inakusudia kufanya marekebisho ya Sheria ya Ardhi ili riba ya kuchelewa kulipa kodi ya pango la ardhi ianze kutozwa baada ya kuisha kwa mwaka wa fedha.

Aidha, Dk Mabula amesema wizara imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa wananchi yanayohusiana na kucheleweshewa, kulipwa pungufu au kutolipwa fidia.

“Nasisitiza taasisi za Serikali na kampuni binafsi kulipa fidia kwa wakati ili kuepusha ulipaji wa riba na malalamiko yanayotokana na ucheleweshaji wa ulipaji fidia,”amesema.

Amesema Serikali haitaruhusu utwaaji wa ardhi bila kulipa fidia.