Wanaocheza michezo ya kubahatisha wapewa ujumbe

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), James Mbalwe

Muktasari:

  • Wewe ni mchezaji wa michezo ya kubahatisha, umewahi kucheza, ukashinda na ukasumbuliwa kulipwa ushindi wako? Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT) inasema ikikutokea wafuate wao.

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), James Mbalwe amewashauri watu wanaokutana na changamoto ya kudhulumiwa baada ya kushinda kwenye michezo ya kubahatisha kupeleka malalamiko yao kwenye bodi hiyo, ili wasaidiwe kwa urahisi zaidi.

 Amesema wapo wanaokwenda Polisi, lakini huko watasikilizwa na kwa kuwa wengi hawana uelewa na michezo ya kubashiri matokeo, watawarudisha kwenye bodi.

Mbalwe amesema hayo jana Jumatano, Machi 6, 2024 katika kikao baina ya bodi hiyo, wahariri na waandishi wa habari kilichoandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina na kufanyikia jijini Dar es Salaam.

"Ni rahisi zaidi kupata msaada ukija kwetu kama umedhulumiwa, tumekuwa tukipata changamoto hizi kutoka kwa wachezaji mbalimbali na tunazishughulikia hadi wanalipwa," amesema.

Akitolea mfano baadhi ya washindi wa Novemba 2023, amesema walipata ushindi mkubwa na bodi hiyo iliwasimamia wote wakalipwa, mkurugenzi huyo amesema hiyo ni sehemu ya majukumu yao.

"Kudhulumiwa wachezaji ni moja ya changamoto tunazokabiliana nazo," amesema.

Amesema changamoto nyingine ni baadhi ya watu kuanzisha michezo hiyo kienyeji bila leseni na baadhi kukiuka masharti ya leseni ya michezo hiyo.

"Hawa huwa tunawakamata na kuwapeleka kwenye sheria," amesema.

Baadhi ya washiriki katika semina hiyo

Semina hiyo imelenga kutambulisha na kujua majukumu ya bodi hiyo sanjari na kukumbusha changamoto na mafanikio kwenye taasisi za umma katika utawala wa Rais Samia Suluhu Hassan utakaofikisha miaka mitatu Machi 19, 2024.

Mbalwe amesema michezo ya kubahatisha ni burudani, haipaswi kubadilishwa na kuwa chanzo kikuu cha mapato na hilo wamekuwa wakilipazia sauti mara zote.

"Bahati nzuri wengi wameanza kuelewa, wanafanya kazi na kubeti kama sehemu ya burudani, tangu bodi hii imeanzishwa Julai mosi, 2003, changamoto zilikuwepo, tumeendelea kuzisimamia kwa ufanisi hadi sasa.

Akizungumzia mafanikio, amesema,"Kumekuwa na ongezeko la kodi kutoka Sh33.6bilioni 2016/17 hadi Sh 170.4 bilioni 2022/23.

"Mwaka huu makisio ni kukusanya Sh200 bilioni, kwa sasa katika kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka jana kodi iliyopatikana ni Sh108 bilioni, makisio ni kukusanya bilioni 200 mwaka huu.

Amesema hivi sasa, kampuni 91 zimesajiliwa kufanya shughuli za michezo ya kubahatisha nchini.

"GBT imekuwa ikichangia kwenye mfuko mkuu wa Serikali na kwenye maendeleo ya jamii, sekta inakuwa na inaafanya vizuri kwenye burudani, biashara na uchumi.

"Bodi imetoa ajira rasmi na zisizo rasmi 25,000 mpaka, pia asilimia tano ya kodi ya sports betting (kubeti kwenye michezo) inakwenda BMT (Baraza la Michezo la Taifa) kuendeleza michezo nchini," amesema.

Mkurugenzi huyo amesema,"wakati wa ukoloni, michezo hii ilikuwepo na ililenga kukusanya fedha kujenga huduma za jamii, hapa kwetu kabla ya GBT kulikuwa na Shirika la Bahati Nasibu ya Taifa,”

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa Huduma wa GBT, Daniel Olesumaiya amesema mchakato wa kurejesha bahati nasibu ya taifa unaendelea.

"Mwezi huu tukihitimisha mchakato, mwaka ujao fedha tutaanza kuisikia bahati nasibu taifa, ambayo sheria inataka asilimia 50 ya mapato yake kusaidia michezo.

Akizungumzia uwekezaji kwenye michezo ya kubahatisha, Olesumaiya amesema inategemea inawekeza kwenye mchezo gani.

"Sera inasema kwa mwekezaji kutoka nje ya nchi, awe na kuanzia dola 500,000 na wa ndani dola 300,000.

"Kwenye Bahati nasibu ya taifa ni dola milioni 20, inategemea na uwekezaji, kwenye Cassino ni kama dola milioni moja,” amesema