Wanaodaiwa kuiba Sh790 milioni upelelezi bado, Jamhuri yasubiri ripoti
Picha na Mtandao.
Muktasari:
- Wanadaiwa kati ya Agosti 2, 2022 na Novemba 25, 2025, ndani ya Mkoa wa Katavi na Dar es Salaam na Tabora washtakiwa kwa nia ya ovu waliongoza genge la uhalifu kwa kutakatisha fedha na wizi.
Dar es Salaam. Jamhuri katika kesi ya wizi inayomkabili aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya Premium Active Tanzania Ltd, Juma Adolick (35) pamoja na Lina Philipo, maarufu Linna Filipo, imedai inasubiri ripoti ya kiusalama ya kimtandao kutoka kwa mpelelezi, ili kukamilisha upelelezi.
Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Chalo ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo, Jumanne Julai 14, 2026, kesi hiyo ilipotajwa.
Adolick ambaye ni mkazi wa Bomba mbili, Ukonga na Lina mkazi wa Kitunda, wakikabiliwa na mashtaka 22 yakiwemo ya wizi na kutakatisha fedha.
Washtakiwa hao wanadaiwa kuiba Sh493 milioni na kutakatisha fedha kiasi cha Sh790 milioni na kwamba kiasi hicho cha fedha walikitumia kununulia nyumba sita zilizopo wilayani Ilala, Urambo na Mpanda.
Wakili Chalo ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hassan Makube.
"Upelelezi wa kesi hii haujakamilika na kwamba tunasubiri ripoti ya kiuchunguzi ya mtandao kutoka kwa mpelelezi, hivyo kwa sababu hiyo tunaomba mahakama itupangie tarehe nyingine," aliomba Wakili Chalo.
Hakimu Makube baada ya kusikiliza maelezo hayo, aliahirisha kesi hadi Julai 28, 2026 kwa kutajwa.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili, halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa walifikishwa mahakamani hapo Julai 2, 2026 na kusomewa kesi ya uhujumu namba 14707 ya mwaka 2026.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kuongoza genge la uhalifu wa kupangwa tukio wanadaiwa kulitenda kati ya Agosti 2, 2022 na Novemba 25, 2025, ndani ya mikoa ya Katavi, Dar es Salaam na Tabora, ambapo kwa nia ya ovu waliongoza genge la uhalifu kwa kutakatisha fedha na kufanya wizi.
Shtaka la pili ni wizi linalomkabili Adolick pekee yake, ambapo Inadaiwa kati ya Julai 11, 2023 na Agosti 22, 2023 mkoa wa Katavi, akiwa mtumishi wa kampuni ya Premium Active Tanzania Ltd aliiba Sh493 milioni.
Shtaka la tatu hadi la 22 ni kutakatisha fedha yanayowakabili washtakiwa wote.
Miongoni mwa mashtaka ya kutakatisha fedha ni kwamba kati Julai 1, 2023 na Julai 27, 2023 pamoja na Agosti 30, 2023 hadi Oktoba 2, 2023 Lina alimuwezesha Adolick kupata Sh790 milioni kwa kumuweka fedha hizo kupitia akaunti ya Lina katika benki ya CRDB tawi la Gongolamboto na Mpanda.
Pia, wanadaiwa katika kipindi cha Februari 18, 2023 na Novemba 25, 2025 washtakiwa wote walijipatia nyumba sita ambazo hazijapimwa, zilizopo Mpanda, mkoani Katavi, Bombambili Wilaya ya Ilala na Urambo mkoani Tabora, wakati wakijua kuwa fedha zilizotumika kujengea nyumba zilitokana na kosa tangulizi la kuongoza genge la uhalifu na wizi.