Wanaonyanyasa wanawake kufuatiliwa kwenye masoko

Muktasari:

Mbinu hiyo ya mapambano imepokelewa vizuri na wananchi wanaokerwa na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake vikiwamo vya kuwaghasi, kuwakejeli na hata kuwashikashika bila ridhaa zao ambapo baadhi wameilezea kuwa inafaa kusambazwa nchini kote.

Mapambano dhidi ya ukatili kwa wanawake yamechukua sura mpya baada ya kuelekezwa kwenye masoko ambako wengi hufika kwa ajili ya kujipatia mahitaji ya familia zao.

Mbinu hiyo ya mapambano imepokelewa vizuri na wananchi wanaokerwa na vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wanawake vikiwamo vya kuwaghasi, kuwakejeli na hata kuwashikashika bila ridhaa zao ambapo baadhi wameilezea kuwa inafaa kusambazwa nchini kote.

Wafanyabiashara katika Soko la Mwaloni jijini hapa wamekiri kuwapo kwa changamoto nyingi zinazowakabili wanawake na kwamba, zaidi ni upungufu wa matundu ya vyoo kwa kuwa vilivyopo havitoshi.

Hilda Gozbert anayejishughulisha na uuzaji dagaa katika soko hilo lililopo Kirumba alisema ni jambo la fedheha choo kimoja kutumiwa na wanaume na wanawake na kuitaka Serikali ione umuhimu wa kuongeza matundu ya vyoo katika soko hilo.

Akizungumzia hali hiyo, Mwenyekiti wa soko hilo, Fikiri Magafu alisema licha ya vyoo vilivyopo kuwa bora, lakini havitoshi kwa kuwa wanaume hulazimika kutumia vya wanawake kutokana na idadi yao kuwa kubwa ikilinganishwa na wanawake. “Si kwamba wanatumia choo kimoja, hapana. Isipokuwa wanaume wakifika sehemu yao wakakuta pamejaa hujihifadhi kwa wenzao,” alisema Magafu.

Akizindua mradi huo juzi, Ofisa Ufuatiliaji na Tathmini wa Shirika la Equality for Growth (EFG), Samora Julius alisema lengo lao ni kufuatilia kwa kina masuala ya haki kwa wanawake katika maeneo hayo na wataanza katika Soko Kuu la Mwanza, Mkuyuni, Igogo, Kirumba, Mwaloni na Mlango Mmoja.