Wanaotumikisha wahamiaji Kigoma wapewa siku saba
Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, wakati akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano, Juni 17, 2026 ofisini kwake katika Mtaa wa Mnarani mkoani Kigoma.
Muktasari:
- Hatua hiyo inajiri baada ya ongezeko la wahamiaji wasio na vibali huku kukiwa na tishio la ugonjwa wa Ebola nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Kigoma. Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, ametoa siku saba kwa wananchi na wafanyabiashara wanaowatumia wahamiaji kutoka nchi jirani wasio na vibali halali vya kuishi na kufanya kazi nchini kuwarejesha kwao kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Balozi Sirro amesema katika siku za hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la wahamiaji haramu wanaoingia mkoani humo na kuajiriwa katika shughuli mbalimbali za kiuchumi, ikiwamo kilimo, nyumba za kulala wageni na baa.
Amesema mbali na kuvunja sheria za uhamiaji, uwepo wa wageni hao bila kufuata taratibu unaweza kuhatarisha usalama wa afya ya jamii, akieleza kuwa wanaweza kuwa chanzo cha kuenea kwa magonjwa ya mlipuko, ikiwamo Ebola, na hivyo kuliingiza Taifa katika changamoto kubwa ya kukabiliana na maradhi hayo.
Wito huo ameutoa leo Jumatano, Juni 17, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake katika Mtaa wa Mnarani mkoani Kigoma.
Aidha, amewataka viongozi wa mitaa, watendaji wa vijiji na kata kutoa taarifa kwa mamlaka husika pindi wanapobaini uwepo wa wageni wasiokuwa na vibali halali katika maeneo yao.
Balozi Sirro amesema wageni wengi huvutiwa kuingia nchini kutokana na fursa mbalimbali zilizopo, zikiwamo ajira katika sekta ya kilimo, malipo mazuri ya kazi, huduma bora na upatikanaji wa bidhaa mbalimbali.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa wageni wote wanaotaka kuishi au kufanya kazi nchini wanapaswa kufuata taratibu na sheria za uhamiaji zilizowekwa na Serikali.
‘’Sasa ninachowaambiwa kwamba kwenye baa zetu, kwenye hoteli zetu, kwenye maduka yetu na hasa hapa Kigoma mjini, wamejaa wahamiaji haramu, hii ni kutukosesha heshima kama Watanzania.
‘’Sasa wale wote ambao wanawahifadhi au wanawatumia hawa wahamiaji haramu, nawapa wiki moja wawaachishe kazi na wawarudishe kwao vinginevyo tutamkamata yule anayefanya kwenye hoteli yako au kwenye gesti yako tutakupeleka mahakamani kwa kuhifadhi mhamiaji haramu,’’ amesema.
Aidha Jumapili Juni 14,2026, wahamiaji haramu 95 kutoka mataifa ya Burundi, Rwanda na DRC walikamatwa na maofisa wa uhamiaji kanda maalumu Mkoa wa Kigoma.
Katika taarifa iliyotolewa na Naibu Ofisa Uhamiaji mkoani humo, Jeremiah Mwakibinga, wahamiaji hao walikamatwa katika nyumba za kulala wageni, Stendi Kuu ya mabasi pamoja na kumbi za starehe zilizopo manispaa ya Kigoma Ujiji.
Akitoa taarifa kuhusu hali ya ugonjwa wa Ebola, Balozi Sirro amesema hakuna maambukizi yaliyothibitika kuwepo mkoani humo huku akisisitiza kuwa Serikali ya mkoa inaendelea kushirikiana na wataalam wa afya kuchukua hatua zote muhimu za tahadhari dhidi ya ugonjwa huo.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk Damas Kayera amesema mkoa umeimarisha vituo vya kufanya uchunguzi kwa ajili ya wageni wanaoingia nchini kupitia Mkoa wa Kigoma sambamba na kuendelea kutoa mafunzo ya utayari wa kimatibabu kwa wataalam wa afya kwa halmashauri zote za mkoa huo.