Wanasiasa wanaochochea migogoro ya ardhi waonywa

Muktasari:
- Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula amewaonya baadhi ya wanasiasa watakaoleta taharuki na kusababisha uchochezi kwa wananchi katika zoezi la utatuzi wa matumizi ya migogoro ya ardhi katika vijiji 975 nchini.
Arusha. Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angelina Mabula amewaonya baadhi ya wanasiasa watakaoleta taharuki na kusababisha uchochezi kwa wananchi katika zoezi la utatuzi wa matumizi ya migogoro ya ardhi katika vijiji 975 nchini.
Dk Mabula amesema hayo leo Alhamisi Aprili 21, 2022 mkoani Arusha wakati yeye na timu yake ya Mawaziri wa Wizara za kisekta wakitoa mrejesho wa maamuzi ya Baraza la Mawaziri kwa viongozi wa mkoa na wilaya kuhusu migogoro ya matumizi ya ardhi.
Amesema wakati wa utatuzi mwanasiasa atakayeharibu utatuzi wa migogoro hiyo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
"Hatutakubali mwingiliano wowote wa kisisasa kukwamisha hili, mwanasiasa atakayeleta taharuki kwa wananchi serikali itamshughulikia hakikisheni mnadhibiti chokochoko na ambaye ataonyesha uchonganishi toeni taarifa kwani hatuhitaji kuleta taharuki kwa wananchi wakati utekelezaji unaendelea,"amesema
Dk Mabula amesema ziara hiyo ya mkoa kwa mkoa ya kushughulikia migogoro ya ardhi kwenye vijiji 975 ambavyo baraza la mawaziri limeridhia marekebisho.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo, Anthony Mavunde ametoa rai kwa Wakala wa Mbegu(ASA)na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) kupima maeneo yao na kuyaendeleza ili kuweza kufanya mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa ajili ya shughuli za kilimo.
Naye Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Khakis Hamza Chilo amesisitiza utunzaji wa mazingira ni muhimu ili kulinda uoto wa asili.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amesema ni muhimu maeneo ya malisho kutengwa na kulindwa ili kupunguza migogoro inayojitokeza baina ya wakulima na wafugaji.