Wanawake hawataki kuitwa mama

Muktasari:

  • Siku moja niliona mwanamke mmoja mashuhuri anagombana na watu mtandaoni kwa sababu ya kwanini watu wanamuita Rais Samia Suluhu Hassan ‘mama’. Hoja zake zikiwa, kumuita Samia Suluhu mama ni kama vile kumpunguzia majukumu makubwa ya urais aliyonayo, pia ni sawa na kumletea mazoea.

Siku moja niliona mwanamke mmoja mashuhuri anagombana na watu mtandaoni kwa sababu ya kwanini watu wanamuita Rais Samia Suluhu Hassan ‘mama’. Hoja zake zikiwa, kumuita Samia Suluhu mama ni kama vile kumpunguzia majukumu makubwa ya urais aliyonayo, pia ni sawa na kumletea mazoea.

Wakati nasoma hoja zake ilibidi niache kwanza, niweke simu pembeni, nisimame, nitembee hatua kumi, hapa mpaka pale ili nione kama nitafika salama bila kuanguka wala kupepesuka, maana nilikuwa na wasiwasi kwamba inawezekana hajaandika hivyo ila macho yangu ndiyo yanasoma hivyo kwa sababu labda nimelewa. Nikafika salama, nikagundua kuwa ni kweli aliandika hivyo, SIJALEWA.

Siku nyingine tena, nikaona mwanamke mwingine mashuhuri mtandaoni ameweka picha ya meseji alizokuwa akitumiana na mtu ‘inbox’. Huyo mtu alimuandikia huyu mwanamke mashuhuri na ujumbe wake wa salamu ulisomeka “Mama habari”

Kwa hiyo huyo mwanamke akachukua hiyo meseji na kuiweka hadharani na kuandika, mtu unapata wapi nguvu za kuniita mimi mama?

Watu wengi wakashangaa kwenye comment, wakawa wanamuuliza kuna tatizo gani mtu kukuita mama? Akawajibu mimi sio mama yake, kila mtu ana mama mmoja tu, hivyo hupaswi kuita watu wengine mama.

Nilipokuwa nasoma majibu yake nilikuwa nakunywa soda, ikabidi nigeuza ile chupa upande wa nyuma nisome vilivyotumika kutengeneza hii soda, labda huenda kuna kilevi chochote kinachonifanya nisome vibaya nilichokuwa nakisoma mtandaoni. Lakini kwenye chupa ya soda hakukuwa na neno ‘alcohol’ kwa hiyo hakukuwa na kilevi, nilichokisoma kilikuwa ni sahihi kabisa.

Kwa kweli, matukio haya mawili yananifanya nisielewe ni nini kimetokea kwa wanawake. Je hawajivunii tena kuwa mama? Kuna shida gani mtu kuitwa mama?

Ukiniuliza mimi, hakuna cheo kikubwa duniani kuzidi cheo cha wazazi. Mpaka leo tunamuita Julius Nyerere Baba wa Taifa. Tungeweza tu kumuita Rais msataafu au mpigania uhuru, lakini kwa nini tunamuita ‘BABA’? Kwa sababu vyeo hivi viwili vina uzito mkubwa sana na mtu akikuita hivyo heshima.

Nenda kasome vitabu vyote vya dini uone mama na baba wanavyotukuzwa, halafu wewe unakuja kuitwa majina yaliyotukuka unakataa? Labda kama unaona utukufu haufanani na wewe.

Tena kwenye dunia hii ya leo ya vijana wasiokuwa na adabu, mtu akikuita mama unatakiwa umpe na zawadi ikiwezekana kwa maana amekuheshimu, anadhani unaweza kuwa hadhi sawa na mama yake. Tena hususan kwa mtu usiyemjua, akikuita mama kwa mara ya kwanza mnakutana maana yake hivyo ndivyo jinsi anavyokuheshimu, kama mama yake. Angeweza kukuletea uhuni, angeweza kukuita majina ya kihuni au hata jina lako, lakini kakuheshimu kakuita mama. Kiukweli wanawake wana masharti sana siku hizi, ni kama vile hakuna jema tunaweza kufanya kwa ajili yao, kila tunachofanya tunakosea. Kwanini?