Wanawake kufanyiwa upasuaji kurekebisha maumbile bure

Muktasari:

  • Wanawake wenye majeraha makubwa ya moto, ajali, ukatili wanatarajia kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha maumbile yao bure chini ya ufadhili wa taasisi tatu ikiwamo Hospitali ya Aga Khan kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili pamoja na timu ya madaktari kutoka Ughaibuni.

Dar es Salaam. Hospitali ya Aga Khan kwa kushirikiana na Shirika la Reconstructing Women International (RWI) na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), inatarajia kufanya upasuaji kurekebisha maumbile kwa wanawake 25 kutoka maeneo tofauti nchini.

Upasuaji huo unaotarajiwa kuanza kesho Novemba 28 hadi Desemba 2, 2023 jijini Dar es Salaam katika hospitali ya Aga Khan, unalenga kurejesha uwezo wa kutembea kwa watu hao.

Programu hiyo itasimamiwa na timu ya madaktari wa upasuaji wa kimataifa wa kurekebisha maumbile kutoka Marekani, Canada, na Ulaya wakishirikiana na madaktari wa hospitali za Aga Khan Dar es Salaam, Muhimbili, Bugando, na Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Novemba 27, 2023 jijini hapa, daktari Mwandamizi wa upasuaji kutoka Aga Khan, Dk Athar Ali, amesema programu hiyo ambayo kwa mwaka huu ni ya nane tangu inalenga kurejesha utendaji wa kimwili ili kuwezesha na kuboresha maisha ya wanawake Tanzania.

Dk Ali amesema licha ya upasuaji kwa wagonjwa pia madaktari nchini watapata faida ya kupata utaalamu sekta ya upasuaji.

"Katika awamu saba zilizopita kati ya mwaka 2016-2022, wataalamu 16 wakiwemo madaktari wa upasuaji wa kurekebisha maumbile, madaktari wa upasuaji wa kawaida, na madaktari wanafunzi kutoka hospitali za umma (Muhimbili, Bugando, Mnazi Mmoja Zanzibar, na Aga Khan, Dar es Salaam wamepata mafunzo kupitia programu hii.” amebainisha.

Daktari bingwa wa upasuaji na kiongozi wa timu ya RWI, Dk Andrea Pusic amesema ushirikiano uliopo kati ya taasisi hizo umeleta ongezeko la utaalamu na uwezo wa madaktari wa upasuaji kurekebisha maumbile.

"Kwa pamoja, tumeweza kuhudumia mamia ya wanawake na wasichana waliojeruhiwa ili kuboresha utendaji wa kimwili na mwonekano wao," amesema.

Naye Daktari bingwa wa upasuaji katika Hospitali ya Aga Khan, Dk Aidan Njau amesema changamoto iliyopo kwa watu hao ni kukosa kujiamini baada ya kupata matatizo.

"Mtu anashindwa kujiamini anashindwa hata kwenda sokoni, kanisani au msikitini. Sasa msaada huu unawarudishia kujiamini.

"Mbali na programu hiyo lakini pia tunapata utaalamu kutoka kwa madaktari kutoka nje kwasababu wamekuja na teknolojia ya hali ya juu, ningependa kuchukua fursa hii kuwakumbusha Watanzania kuitumia vizuri ambayo kwa kawaida ni ghali lakini sasa inapatikana bure," amesema.

Naye, Mkuu wa Upasuaji wa kurekebisha maumbile kutoka Muhimbili, Dk Edwin Mrema, amesema: “Sisi madaktari wa upasuaji wa kurekebisha maumbile tunafurahia zaidi kazi yetu pale tunaposaidia kurejesha tabasamu na hali ya kujiamini iliyopotea kwa wanawake na watoto," amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Aga Khan, Sisawo Konteh, amewashukuru wahisani kwa michango yao ya kifedha kwa ajili ya kuunga mkono program hiyo kwa miaka mingi.

 Amesema miongoni mwa mambo aliyojifunza katika miaka iliyopita ni kuongeza usaidizi wa afya ya akili kwa wagonjwa baada ya kufanyiwa upasuaji ili kukidhi mahitaji yao ya kisaikolojia na kuwasaidia kurejea katika maisha yao ya kawaida.