Wanawake waeleza elimu ya mabadiliko tabianchi invyowezesha kukabili changamoto
Mkazi wa Kivule jijini Dar es Salaam, Veronica Julius akieleza namna mbinu za kukabiliana athari za mabadiliko ya tabia nchi zilivyobadili maisha ya jamii yake.
Muktasari:
- Waeleza elimu ya athari za mabadiliko ya tabianchi inawasaidia wanawake kubadili changamoto kuwa fursa
Dar es Salaam. Miaka michache iliyopita, Veronica Julius alikuwa akitazama kwa huzuni mazao yake yakiharibiwa na mvua kubwa au kunyauka kutokana na ukame. Leo, mkazi huyo wa Kivule wilayani Ilala anazungumza kwa matumaini, akisema elimu ya mazingira imemsaidia kuona fursa mahali ambapo wengi huona changamoto.
Simulizi yake ni miongoni mwa ushahidi unaoonyesha jinsi maarifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi yanavyoweza kusaidia jamii, hususan wanawake na wasichana, kukabiliana na athari zinazozidi kujitokeza kila mwaka.
Akizungumza Juni 23, 2026, wakati wa warsha iliyoandaliwa na Shirika la My Legacy kwa lengo la kusikiliza maoni ya wanawake kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi na namna wanavyokabiliana nazo, Veronica alisema maisha yake yalibadilika baada ya kupata elimu ya mazingira.
“Mvua zikiwa nyingi, mashamba yetu yanajaa maji na kushindwa kulimika. Kiangazi kikifika, ardhi hukauka haraka kwa sababu ni ya mchanga. Tulikuwa tunapoteza mazao na kipato,” amesema.
Kwa kuwa kilimo ni moja ya vyanzo vyake vikuu vya mapato, hali hiyo ilimlazimu kutegemea zaidi kazi za vibarua ili kuendesha maisha ya familia yake.
Hata hivyo, amesema baada ya kushiriki mafunzo mbalimbali kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi, alipata uelewa wa namna ya kujenga ustahimilivu dhidi ya athari za mabadiliko hayo na kutafuta njia mbadala za kujiongezea kipato.
Kupitia mafunzo hayo, Veronica na wanawake wengine waliunda vikundi na kuanzisha shughuli za mazingira kupitia klabu za jinsia zinazofanya kazi katika eneo la Kivule.
Moja ya shughuli hizo ni kampeni ya “Taka Sifuri”, inayolenga kubadili mtazamo wa wananchi kuhusu taka na kuzigeuza kuwa rasilimali za kiuchumi.
“Watu wengi wanafikiri taka ni kitu cha kutupa. Lakini tumegundua kuwa taka ni mali. Zinaweza kutumika kutengeneza bidhaa mbalimbali au hata kuongeza kipato cha familia,” amesema.
Kutokana na ubunifu huo, makopo ya plastiki yaliyokuwa yakitupwa ovyo sasa yanatumika kama vyombo vya kupandia maua, huku taka nyingine zikikusanywa na kurejelewa kwa matumizi mbalimbali ya uzalishaji.
Mbali na kusaidia kutunza mazingira, hatua hiyo imeanza kuwajengea wanawake uwezo wa kujipatia kipato na kupunguza athari za uchafuzi wa mazingira unaochangia mabadiliko ya tabianchi.
Mratibu wa Programu wa Shirika la My Legacy, Amina Mtengeti, amesema wanawake ni miongoni mwa makundi yanayoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi kutokana na majukumu yao ndani ya familia na jamii.
Amesema moja ya changamoto kubwa inayotokana na mabadiliko hayo ni upungufu wa maji unaosababishwa na ukame au mabadiliko ya mifumo ya mvua.
“Kunapokuwa na uhaba wa maji, jukumu la kutafuta maji mara nyingi huwaangukia wanawake na watoto wa kike. Hivyo, wanatumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli nyingine za maendeleo,” amesema.
Kwa mujibu wa Amina, athari za mabadiliko ya tabianchi haziishii kwenye uchumi wa kaya pekee, bali pia huathiri afya na ustawi wa wanawake na wasichana.
Ameeleza kuwa ukosefu wa maji safi unaweza kuathiri usafi binafsi na kuongeza hatari ya magonjwa mbalimbali, hususan kwa wasichana wakati wa hedhi.
“Ndiyo maana elimu kuhusu mabadiliko ya tabianchi ni muhimu. Tunahitaji jamii zielewe athari hizi na kujifunza namna ya kujenga ustahimilivu kabla hazijawa kubwa zaidi,” amesema.
Amesema kuwa kuwapa wanawake na wasichana maarifa kuhusu tabianchi si tu kunawasaidia kujikinga dhidi ya madhara ya mazingira, bali pia kunawapa uwezo wa kubaini fursa za kiuchumi zinazoweza kuibuliwa kupitia shughuli za uhifadhi wa mazingira.
Kupitia mradi wa Mialo ya Kijani unaotekelezwa na My Legacy kwa kushirikiana na Hadithi House na kufadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia programu ya Vijana Art Works, wanawake na wasichana kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam wamekuwa wakipata nafasi ya kueleza uzoefu wao, kujifunza mbinu za kukabiliana na athari za tabianchi na kushiriki katika shughuli zinazochangia uhifadhi wa mazingira.