Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanawake wabeba mzigo wa mabadiliko ya tabianchi kimyakimya

Mratibu wa miradi wa shirika la Mylegacy Amina Mtengeti akizungumza wakati wa utambulisho wa mradi wa Miale ya Kijani unaolenga kupata sauti za wanawake kuhusu namna wanavyokabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Muktasari:

  • Katika jamii nyingi nchini, wanawake ndio wanaohusika zaidi na shughuli zinazotegemea rasilimali za asili kama vile kutafuta maji, kuni na kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha familia, hali inayowafanya kuwa mstari wa mbele kukumbana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Dar es Salaam. Wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zikiendelea kuathiri maisha ya wananchi watu kwa namna mbalimbali, imeelezwa kuwa wanawake wameendelea kubeba mzigo mkubwa wa kukabiliana na hali hiyo huku mchango wao ukiwa hauonekani vya kutosha katika mijadala ya sera na maamuzi ya maendeleo.

Katika jamii nyingi nchini, wanawake ndio wanaohusika zaidi na shughuli zinazotegemea rasilimali za asili kama vile kutafuta maji, kuni na kuhakikisha upatikanaji wa chakula cha familia, hali inayowafanya kuwa mstari wa mbele kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Katika jitihada za kubadili hali hiyo, Shirika la My Legacy limeanzisha mradi unaotumia ubunifu na sanaa kuibua simulizi za wanawake kuhusu namna wanavyokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika maisha yao ya kila siku.

Mradi huo unaojulikana kama “Miale ya Kijani” unatarajiwa kuwapa wanawake nafasi ya kushiriki katika utengenezaji wa filamu fupi itakayoelezea hadithi zao halisi kutoka katika jamii wanazoishi, changamoto wanazokutana nazo na mbinu wanazotumia kuhimili mabadiliko ya mazingira.

Akizungumza leo Jumatatu, Machi 30, 2026 wakati wa kutambulisha mradi huo kwa viongozi wa mitaa na kata kutoka Halmashauri za Kinondoni na Ilala, Mratibu wa Programu wa taasisi hiyo, Amina Mtengeti, amesema lengo la mradi huo ni kubadili simulizi zilizopo katika jamii kwa kuwaweka wanawake kama wahusika wakuu wa hadithi zao wakieleza wanavyoathiriwa mabadiliko ya tabianchi na wanavyojikwamua.

Amesema mradi huo pia unakusudia kuunganisha sekta ya ubunifu inayokua kwa kasi nchini na uhalisia wa maisha ya jamii, hususan katika maeneo ambayo athari za mabadiliko ya tabianchi zinaonekana wazi.

“Kupitia filamu na majadiliano ya kijamii yatakayofanyika katika maeneo mbalimbali, tunatarajia kuchochea mjadala mpana kuhusu umuhimu wa ushirikiano kati ya wanawake na wanaume katika kutafuta suluhisho la changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika hilo, Fortunata Temu, amesema wanawake wamekuwa miongoni mwa makundi yanayoathirika zaidi na mabadiliko ya tabianchi kutokana na majukumu wanayobeba katika familia na jamii.

Amesema athari hizo zinajumuisha ukosefu wa maji safi, ongezeko la magonjwa na hata kuongezeka kwa vitendo vya ukatili vinavyochochewa na mazingira magumu ya kiuchumi na kijamii.

“Ni lazima tukubali kwamba mabadiliko ya tabianchi ni ajenda mtambuka inayohitaji kuangaliwa kwa upana wake, ikihusisha pia masuala ya kijinsia. Ndiyo maana tumekuja na mradi huu ili kusikiliza na kuonyesha sauti za wanawake kuhusu namna wanavyokabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi,” amesema Fortunata.

Akizungumza katika mkutano huo, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Kata ya Kunduchi, Zawadi Mdeme, amesema mradi huo ni fursa muhimu kwa jamii kupata uelewa mpana kuhusu changamoto za mazingira na mchango wa wanawake katika kukabiliana nazo.

Amesema kupitia mradi huo, wanawake watapata jukwaa la kuelezea changamoto wanazokutana nazo kila siku pamoja na mbinu wanazotumia kukabiliana na hali ngumu inayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi.