Wanawake wahamasishwa kugombea uongozi serikali za mitaa

Baadhi ya wanawake Mkoa wa  Mbeya wakiadhimisha Siku ya Wanawake Dunia ambayo kilele chake ni leo Machi 8 mwaka huu. Picha na Hawa Mathias

Muktasari:

  • Manawake mkoa wa Mbeya wamehamasishwa kugombea nafasi za uongozi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu, ikiwa sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani.

Mbeya. Mbunge Viti Maalumu (CCM) mkoa wa Mbeya, Suma Fyandomo amewahamasisha wanawake kujitokeza kuchukua fomu za kuwania nafasi mbalimbali za uongozi kwenye uchaguzi ujao wa serikali za mitaa ili kuchochea mabadiliko ya fursa za kiuchumi nchini.

Fyandomo ametoa wito huo leo Ijumaa, Machi 8, 2024 ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kimkoa imefanyika Mbarali chini ya kaulimbiu isemayo “Wekeza kwa Mwanamke Kuharakisha Maendeleo ya Taifa na Jamii”.

“Wanawake niwatie moyo, msisite, msiogope. Mnatakiwa kuwa mstari wa mbele kuchukua fomu kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama na nje ili kuongeza idadi ya viongozi na kuunga mkono jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan,” amesema.

Amesema umefika wakati wanawake kuwa vinara kwenye masuala ya uongozi, hivyo ni fursa kwao kuonyesha mfano kwa kuchukua fomu kuanzia uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini hivi karibuni.

“Jitokezeni kwa wingi kuchukua fomu, mnaweza. Msirudi nyuma wala kujenga hofu, tunayo mifano ya viongozi wanawake akiwepo Spika wa Bunge na mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson, licha ya nafasi hizo, pia, amekuwa Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU),” amesema.

Amesema anatambua kuwa wanawake ni jeshi kubwa lenye mchango mkubwa kwa Taifa kwa kuonyesha uwezo wa kubeba mzigo kuanzia ngazi ya familia pasipo kuwezeshwa.

Wakati huohuo, akiwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo wilayani Chunya, Fyandomo ametoa mahitaji mbalimbali kwa wagonjwa katika Kituo cha Afya Lupa na viti mwendo vitatu kwa watoto wenye ulemavu.

Akiwa Chunya, Fyandomo amesema ujasiri kwa wanawake ndio nguzo ya kuchangamkia fursa za uongozi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi.

“Tutumie mfano wa Rais Samia Suluhu Hassan, ni mwanamke aliyethubutu  kutangaza  utalii wa ndani wa Royal Tour ambao umezaa matunda kwa kuvuta watalii wengi na kuingiza fedha za kigeni na kukuza uchumi,” amesema.

Mwenyekiti wa maandalizi ya siku ya wanawake duniani mkoani hapa, Bahati Mwampetele amesema halmashauri ya Chunya imewekeza zaidi katika kuwawezesha wanawake kiuchumi katika uanzishaji miradi.

Mbunge wa Lupa (CCM), Masache Kasaka amesema wataendelea kuzungumza na Serikali kuona jitihada za makusudi zinafanywa kuhakikisha utaratibu wa utoaji mikopo ya asilimia 10 unaanza mapema.

“Asilimia kubwa ya wanawake wa Chunya wanajishughulisha na uchimbaji wa madini, lakini changamoto ni mitaji baada ya Serikali kusitisha utoaji mikopo kwenye halmashauri na kuelekeza utaratibu maalumu kupitia taasisi za kifedha,” amesema.

Mjasiriamali, Sekela Joel amesema kupitia siku hii muhimu Serikali itanue wigo wa fursa za kiuchumi kwa kuviwezesha vikundi vya wajasirimali wadogo kwa mikopo nafuu.