Prime
Wanawake waja kasi uvutaji wa sigara-Utafiti

Dar es Salaam.” Uvutaji wa sigara ni hatari kwa afya yako” ni tangazo marufu lililopo maeneo mengi.
Licha ya uwepo wa matangazo hayo na kutolewa kwa elimu katika vyombo vya habari, kuhusu athari za matumizi ya sigara, baadhi ya wanawake wameendelea kujiingiza katika uvutaji wa sigara huku wanaume wakipungua; utafiti unaeleza.
Ripoti ya utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (THDS) ya mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), inaeleza kuwa kiwango cha wanawake wanaovuta sigara ni asilimia moja.
Kiwango kimeendelea kubaki hivyo licha ya idadi ya watu katika vipindi tofauti vya kuongezeka, jambo linaloashiria kuongezeka wa idadi ya wanawake wanaovuta sigara kati ya 2017 na 2022.
Kabla ya takwimu hizo za NBS, mwaka 2021 shirika la Afya Duniani (WHO) likishirikiana na Serikali ya Tanzania walitoa takwimu ya ongezeko la wanawake kuvuta sigara, kwa kueleza kuwa mwaka 2012 walikuwa asilimia 2.9 na mwaka 2018 walikuwa asilimia 3.2.
Kwa mujibu wa takwimu za NBS wavutaji sigara wanapungua, kadri kiwango cha elimu kinavyoongezeka. Matumizi makubwa ya tumbaku yapo katika mikoa ya Mashariki ambayo ni Kigoma, Tabora na Katavi kwa asilimia 15 huku mikoa ya Kaskazini ambayo ni Arusha na Kilimanjaro ikiwa kwa asilimia 14.

Watumiaji wazungumza
Rose Majid, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam, alisema matumizi ya sigara kwa wanawake yameongezeka kutokana na mtindo wa maisha wanayoishi huku wengine wakiiga kutoka kwa marafiki walionao.
“Ukiona mwanamke anavuta sigara kuna uwezekano akawa mtumiaji wa pombe pia ni wachache wanavuta sigara peke yake hii inasababishwa na mazingira pamoja na marafiki tunaokuwa nao,” alisema Rose na kuongeza:
“Marafiki wana ushawishi mkubwa wa kufanya mambo ambayo wao wanayafanya haiwezekani wenzio wawe wanywaji halafu uwatazame kwa kwenda nao bar. Kwa mwanamke ni ngumu lazima kutakuwa na ushawishi ni sawa na sigara ipo siku utajaribu tu.’’
Alisema ana miaka 20 sasa anatumia sigara na ana watoto sita ambao wanne wa kike kati yao mmoja havuti sigara na wawili wa kiume ni wadogo, na kila anapozaa watoto wake wanakuwa na kilo chache kwa sababu ya kuvuta sigara.
“Hospitali walishanikataza kuvuta sigara nikiwa na mimba lakini ilishindikana nahisi kama kuna kitu kinanikaba nisipofanya hivyo na najikuta naumwa kabisa mpaka nivute ndipo napata nafuu,”alisema Rose.
Alisema alishaaambiwa kuhusu athari za matumizi ya sigara alijaribu kuacha lakini ameshindwa na alikuwa mgonjwa, hivyo ilibidi aruhusiwe kuendelea kutumia kwa kuamini kuwa wangempoteza.
Joyce Ndandaro mkazi wa Kigambon, alisema ongezeko hilo si la bahati mbaya bali linatokana na malezi ya wazazi kutozuia watoto kujiingiza kwenye janga la uvutaji wa sigara.
“Nilikuwa namuona mama yangu akivuta sigara hivyo nilikuwa nafuatilia anapoweka sigara zake asipokuwepo nachukua najaribu kuvuta hadi sasa siwezi kuacha ila sitamani mtoto wangu aje kuvuta sigara,”alisema Joyce.
Alisema kwake ilikuwa kama chakula kipindi alipokuwa anasoma alikuwa anavuta kwa kujiiba. Kwa siku alikuwa anavuta moja kidogo asubuhi anazima na atakaporudi shule anamalizia kipisi kilichobaki.
Alisema sigara inatakiwa kukatazwa kama ilivyo bangi kwani inaharibu watoto.
‘‘Hata wakati mwingine kuna watu wanatuma watoto kuwanunulia sigara, hivyo hawaoni kitu cha ajabu wanapokwenda kununua,’’ alieleza.
Pia alisema utandawazi unaharibu watoto kwani watoto wanajifunza kwa kuona hivyo maigizo yanayoonekana kwenye runinga ni chanzo cha watoto kunakiri maisha ya aina hiyo.
Alisema vizazi vya sasa vina tabia ya kuiga mambo mbalimbali ikiwamo uvutaji wa sigara, huku wasanii wakiwa wanahamasisha katika matumizi ya sigara, wakiwa wanafahamu kuwa wao wanatazamwa na kila rika.
“Tamthilia na nyimbo zinazowekwa kwenye runinga zinaweza zikachochea matumizi ya sigara kwa watoto kwa kuamini kuwa maisha yanapaswa kuwa hivyo ya kuvuta sigara na shisha kuwa ni kitu cha kawaida,”alisema.
Joyce alisema siku hizi kumuona mtoto wa kike akivuta sigara si kitu cha kushangaa tena hususani kwenye sehemu za starehe na tabia hizo wanarudi nazo hadi kwenye familia zao na kutengeneza kizazi cha sigara.
Wauzaji wanena
Ongezeko hilo la wanawake kuvuta sigara halijamshangaza Emmanuel Maganga, muuza duka Temeke akidai kuvuta sigara ni starehe kama zilivyo nyingine hivyo kila mmoja anaangalia inayomfaa zaidi.
“Wanawake kuvuta sigara tena hadharani kwa sasa, imekuwa ni fasheni na kila mmoja anaonyesha kile anachoweza kukifanya kwa upande wa starehe na hii inasababishwa na msongo wa mawazo,”alisema na kuongeza:
“Kila siku tunaona matangazo ya kukataza uvutaji wa sigara ni hatari, lakini Serikali inaendelea kuruhusu uzalishaji na kuchukua kodi, hivyo lazima kutakuwa na ongezeko la watumiaji pia.’’
Kwa upande wake, Mussa Massawe mfanyabiashara wa eneom la Mbezi, alisema ni ngumu kudhibiti ongezeko hilo kwa kuwa tumbaku inalimwa nchini licha ya kupadisha kodi kwa kuwa ipo kihalali watu hawaoni shida kutumia.
“Zao linapatikana nchini na linaongeza pato la nchi hivyo tusitegemee kupunguza watumiaji bali kuwepo kwa ongezeko lake na wakipungua upande mmoja basi upande mwingine utaongezeka,”alisema massawe.
Madhara ya sigara
Wataalamu wa afya wanaelezea madhara yanayoweza kutokea kwa wanawake wanapovuta sigara. Daktari wa wanawake katika Kituo cha Afya Tabata, Jumanne Hamad alisema wanawake wanaovuta sigara wanakuwa na nafasi kubwa ya kupata saratani, uwezekano wa kuwa wagumba, mimba kutunga nje ya kizazi, mvurugiko wa homoni, kujifungua watoto wenye uzito mdogo, vifo vya ghafla vya watoto wachanga na matatizo kwenye mfumo wa upumuaji.
Alisema wanawake wamekuwa wakipuuzia ushauri wa madaktari na kuamini kila kitu kwao lazima kifanyike ikiwemo uvutaji wa sigara ambao unakwenda kuharibu mfumo wa uzazi na mifumo mingine ndani ya mwili.
“Jukumu letu madaktari ni kuendelea kutoa ushauri kwa watumiaji wa sigara hususani wakati wa ujauzito ambapo uwezekano wa kuharibu afya ya mtoto aliye tumboni ni mkubwa na tunawashauri kuacha kwa muda kama si kuacha kabisa,”alisema.
Dk Hamad alisema wanawake waliopo kwenye kundi la miaka 15 hadi 40, ni rahisi kupata madhara hayo kutokana na kutumia sigara nyingi tofauti na wale watakaozidi kwani wanapunguza uvutaji.
Upo utafiti pia unaoonyeshawatu wanaovuta sigara moja kwa siku wana uwezekano wa asilimia 50 zaidi kupata magonjwa ya moyo.
Pia watu hao wana uwezekano wa asilimia 30 kupata na kiharusi kuliko watu ambao hawajawahi kuvuta sigara.
Mwenendo wa soko
Ripoti ya Tanzania in Figures 2022 ya NBS, ilionyesha ongezeko la kubwa uzalishaji sigara la asilimia 73 na kufikia sigara bilioni 12.2 mwaka 2022 kutoka bilioni 7.02 mwaka 2021.
Kiwango hicho cha uzalishaji ni kikubwa kwa zaidi ya miaka mitano iliyopita.
Kwa mujibu wa taarifa ya Bodi ya Tumbaku, hadi kumalizika kwa wiki ya Septemba 3, 2023 jumla ya kilo 120,622,761.31 za tumbaku ya mvuke (VFC) zenye thamani ya Sh 701.2 bilioni zilinunuliwa kwa wakulima.
Pia, tani 895. 81 za tumbaku ya Moshi (DFC) zenye thamani ya Sh 3,788, tani 170.59 za tumbaku ya hewa (Burley) zenye thamani ya Sh 659.5milioni na tani73.82 za tumbaku aina ya DAC zenye thamani ya Sh452 milioni, zilinunuliwa kwa wakulima.