Wanawake wanavyofurahia mabadiliko ya nishati safi ya kupikia
Meneja wa Mauzo na Masoko wa kampuni ya Oryx Kanda ya Kaskazini, Gamu Kimollo (kulia) akikabidhi jiko la gesi kwa mmoja wa washindi wa promosheni ya matumizi ya nishati safi mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
- Serikali inalenga kufikia asilimia 80 ya kaya nchini kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.
Moshi. Matumizi ya nishati safi ya kupikia yameendelea kuibua matumaini mapya kwa wanawake mkoani Kilimanjaro baada ya baadhi yao kueleza namna teknolojia hiyo ilivyopunguza gharama, kuokoa muda na kulinda afya za familia.
Wakizungumza leo Septemba 16, wanawake hao waliokuwa miongoni mwa washindi wa promosheni ya kampuni ya gesi ya Oryx, wamesema gesi imekuwa suluhisho la changamoto zilizokuwa zikiwasumbua kutokana na matumizi ya kuni na mkaa.
Kupitia promosheni hiyo, kampuni ya Oryx imekabidhi zawadi mbalimbali ikiwemo pikipiki, majiko ya gesi, seti za sufuria, fedha taslimu na mitungi ya gesi kwa washindi wanne kutoka wilaya mbalimbali za Kilimanjaro.
Mkazi wa Same, Lovenes Madandi amesema kabla ya kutumia gesi alikuwa akikumbana mara kwa mara na matatizo ya kiafya kutokana na moshi wa kuni.
“Faida nyingine ni kuokoa muda. Ukichelewa kutoka kazini, unapika chakula na kinaiva kwa haraka bila shida. Pia haina moshi, ni nishati safi na nzuri kwa afya ya familia zetu,” amesema.
Kwa upande wake, Illen Machenje amesema kupata jiko la gesi ni faraja kubwa kwani linamuwezesha kutekeleza majukumu yake ya kila siku kwa ufanisi.
“Kwa gesi unapunguza muda wa kupikia, ukilinganisha na kuni ambazo unatumia saa nzima. Kwa gesi ni dakika chache tu. Hii ni neema kwa wanawake wengi,” amesema.
Meneja wa Mauzo na Masoko wa Oryx Kanda ya Kaskazini, Gamu Kimollo amesema promosheni hiyo inalenga kuongeza mwamko wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi.
“Leo tumetoa zawadi kwa washindi wanne kupitia kampeni ya Jaza na Ushinde. Dhumuni letu ni kuhamasisha wananchi kuachana na nishati chafu zinazochangia uharibifu wa mazingira na kuathiri afya,” amesema.
Serikali na wadau mbalimbali wamekuwa wakihimiza matumizi ya nishati safi kama gesi, lengo likiwa kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa vinavyosababisha ukataji miti na changamoto za kiafya kwa watumiaji.
Vilevile, Serikali inapambana kupunguza utegemezi wa mkaa na kuni ambapo kwa sasa zaidi ya asilimia 85 ya kaya nchini zinategemea nishati hizo, hali inayochochea ukataji miti na uharibifu wa misitu.
Hata hivyo, inalenga kufikia asilimia 80 ya kaya nchini kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.