Wanawake wanavyokubali vipigo kutoka kwa wenza

Dar es Salaam. Wakati Serikali na jamii zikipambana kukabiliana na ukatili kwa wanawake, ukiwamo wa kimwili, kiuchumi na kisaikolojia; mila na desturi zinatajwa kuchangia vitendo hivyo.

Ukatili huu una athari kubwa katika jamii, ikiwamo kusababisha majeraha, ulemavu, matatizo ya kisaikolojia na hata vifo kwa kinamama, hivyo kuwa kikwazo cha maendeleo yao.

Hata hivyo, Ripoti ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria (TDHS) wa Mwaka 2022 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) hivi karibuni inaonyesha kuwapo wanawake wanaoamini wanastahili kupigwa na waume wao iwapo wataunguza chakula, kutoka bila kuaga, kutelekeza watoto, kuwanyima haki zao za ndoa au kubishana nao.

Loading...

Loading...

Ripoti inaonyesha asilimia 48 ya wanawake wanaamini wanastahili kupigwa ikiwa watafanya mojawapo ya kosa tajwa hapo juu, huku asilimia 32 ya wanaume wanaamini mwanamke anastahili kupigwa akifanya makosa hayo.
Utafiti umefanywa kwa wanawake 15,254 na wanaume 5,763. Ni kutokana na ripoti hiyo, baadhi ya wadau wanasema jamii inatakiwa kubadilika na kuachana na mfumo wa maisha unaochangia vitendo hivyo.
 

Ripoti ya utafiti

Hata hivyo, ripoti inafafanua imani kuwa mwanamke anapaswa kupigwa akifanya makosa hayo ni ndogo kwa wale ambao hawakuwahi kuolewa ikilinganishwa na walio kwenye ndoa.

Asilimia 41 ya wanawake ambao hawajawahi kuolewa walikubali kuwa mwanamume anastahili kumpiga mkewe akitenda mojawapo ya makosa hayo, huku walio kwenye ndoa wakikubaliana na hoja hiyo kwa asilimia 51.
Kwa upande wa wajane, waliotengana na waume wao au kupeana talaka, wanaamini hilo kwa asilimia 49.

Upande wa vijijini, zaidi ya nusu ya wanawake waliofanyiwa utafiti wanaamini wanastahili kupigwa juu ya makosa hayo; huku wanaume wakiwa ni asilimia 34.
Mjini wanawake wanaamini hilo kwa asilimia 41, huku kwa wanaume ikiwa asilimia 26.

Asilimia za wanaoamini wanastahili kupigwa pia zinatofautiana kulingana na viwango vya elimu. Wasiosoma au kuwa na elimu ya shule ya msingi wanaamini ni haki yao kupigwa.

Wanawake watano kati ya 10 walio katika kundi hilo wanaamini wanastahili kupigwa ikilinganishwa na asilimia 36 ya wanawake walio na elimu ya sekondari au ya juu wanaokubaliana na hoja hiyo.

Kipato pia kinachangia wanawake kuamini wanastahili kupigwa. Walio na hali za chini za kiuchumi asilimia 54 wanakubaliana na hoja hiyo, huku asilimia 36 ya walio na kipato cha juu wakikubaliana nayo.
 

Asilimia za makosa, kipigo

Kutoangalia watoto ndiyo sababu ambayo wanawake waliofanyiwa utafiti wanaamini zaidi kuwa wanastahili kupigwa ikiwa watatenda kosa hilo. Asilimia 38 ya wanawake walikubaliana na hoja hiyo, huku wanaume wakikubali kwa asilimia 23.

Asilimia 31 ya wanawake walisema ni haki yao kupigwa ikiwa watatoka bila kuaga, huku wanaume wakikubali hilo kwa asilimia 19.
 

Mtazamo wa jamii, kisaikolojia

Akizungumzia ripoti ya utafiti huo katika mahojiano na Mwananchi, Evelyne Ivan, mkazi wa Dar es Salaam, alisema wapo wanawake wanaoamini kupigwa kunapunguza hasira za wanaume kwa kosa lililotendeka.

“Kwa mfano, mtu akibaini unatoka nje ya ndoa na asiongee chochote wala kukupiga, akuambie mwendelee kuishi unaweza kuhisi anataka kukunyonga ukiwa usingizini, maana hujui anawaza nini. Ukipigwa unaamini hasira zimepungua,” alisema Evelyne.

Mtazamo huo ni tofauti na wa Emmanuel Kimaro, anayesema kipigo si suluhisho, bali kumuacha ili awe huru kufanya anachohitaji.

“Mpaka anafanya kitu anakuwa na sababu, hata umpige vipi hauwezi kutatua changamoto kama sababu itaendelea kuwapo,” alisema Kimaro.
John Ambrose, mtaalamu wa saikolojia, anasema katika uhusiano zinapokosekana mbinu za mawasiliano, kunazalishwa migogoro inayochochea hasira na chuki zinazoweza kusababisha kipigo, udhalilishaji na ukatili.
Anasema pia baadhi ya tamaduni za watu zina namna zinavyowachukulia wanawake na mwanaume.

"Ndiyo maana kuna makabila yanadiriki kusema mwanamke asipopigwa hapendwi, jamii nayo inaamini kuwa hiyo ni njia halali ya utatuzi wa migogoro. Hili lilikuwapo tangu zamani kwamba mtu akizini apigwe," alisema Ambrose.
Hata hivyo, alisema hali hivi sasa ni tofauti; mitazamo ya watu inaendelea kubadilika kutokana na kuelimika.

Alisema uwapo wa vitendo hivyo pia huweza kusababishwa na malezi yanayomkuza mtu, jambo linaloweza kuleta changamoto.
"Unaweza kubadili mitazamo ya watu kupitia malezi na makuzi, ni mafunzo ya kuwajengea stadi wanaoingia katika ndoa kuwapa uwezo wa kukuza familia," alisema.

Alisema kuna haja ya jamii kujengewa utamaduni wa kujua njia na umuhimu wa kuwashirikisha wataalamu wa saikolojia na washauri, ili kupata mbinu stahiki za kusuluhisha migogoro.

Pia alishauri kuboreshwa miundombinu ya kisheria, ustawi wa jamii na kiuchumi.
Haki za binadamu

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, hivi karibuni alikaririwa na gazeti hili akisema ripoti kama hii inatakiwa kufafanua kwa undani zaidi kuonyesha sababu za kwa nini mwanamke anaamini kupigwa ni haki yake.

Hilo ni kutokana na kile alichoeleza kuwa, wakati mwingine mazingira anayokulia mtu humfanya kuona akipigwa ni jambo la kawaida.

“Kama mwanamke amekuwa akiona bibi anapigwa au mama anapigwa na hakuna hatua zilizochukuliwa ataona kinachofanyika ni haki na ataendelea kuishi katika mazingira hayo akiamini akifanya kosa hili anastahili kupigwa,” alisema.

Alisema kitendo hicho kikiendelea na asipokuwapo mtu wa kumuonyesha kuwa si haki, basi suala hilo litaendelea kuonekana la kawaida.

“Ripoti hii inasema kwa nini watu wanaamini lakini si kwamba ndiyo kweli, bali kuna utumwa ambao umekuwapo unaobebwa na kutokuwapo usawa wa kijinsia kwa muda mrefu,” alisema.