Wanawake wataja mbinu kunusuru familia, watoto vitendo vya ukatili

Baadhi ya Wanawake Kata ya Msangani Halmashauri ya Mji wa Kibaha Mkoa wa Pwani wakichangamsha Sherehe ya maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika Msangani Mkoani Mjini Kibaha, Picha na Sanjito Msafiri

Kibaha. Wanawake Kata ya Msangani Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mkoa wa Pwani wameiomba Serikali kukomesha vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea kwa baadhi ya familia jambo linaloathiri shughuli kiuchumi na kusababisha malezi ya watoto kuwa duni.

Kutokana na hali hiyo wanawake hao wameiomba Serikali kuongeza nguvu katika kuendelea kuelimisha juu ya sheria mbalimbali zinazomkandamiza mwanamke ili kuwe na uelewa mpana na kuweka kizazi chenye usawa kwa jamii yote.

“Baadhi ya wanawake hawafahamu haki zao za ndoa na kisheria kama vile talaka, mirathi na sheria ya ardhi ya mwaka  1999. Hivyo tunaiomba Serikali iliangalie hili kwa kutuletea wataalamu wawe wanatoa elimu kwa kundi hilo," amesema Mwajuma Makuka.

Makuka ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake Kata ya Msangani amesema kuwa mbali na hilo pia athari nyingine ni kukithiri kwa mimba za utotoni, vitendo ambavyo kwa baadhi ya familia vimekuwa vikitokea na wahusika kumalizana kwa njia za mazungumzo bila kwenda kwenye vyombo vya sheria hivyo kufanya watuhumiwa wa mambo hayo kuona kuwa hakuna sheria inayowabana na kuendelea kujihuisha na uovu huo.

Kwa upande wake, Suzana Daudi amesema kuwa vitendo vya ubakaji vimekithiri kwenye maeneo yao na Ili kukabiliana na hali hiyo kinachotakiwa kufanyika ni ushirikiano baina ya jamii na Serikali hasa kufichua maovu hayo.

"Mimi ni mmoja wa watu waliokumbwa na shida hiyo, mwanangu alibakwa na nikachukua hatua ya kuripoti tukio hilo, nashukuru sheria ilifanya kazi yake na mpaka sasa aliyetenda kosa hilo amehukumiwa yukó jela," amesema.

Kwa upande wake Lilian Simon wa Kituo cha kulea Watoto Yatima cha Shalom Oprphanage, amesema kuwa ili kuwa na Taifa lenye upendo na amani kuna umuhimu wa jamii kuanza kuwaandaa watoto wadogo kwa kuwapa maelezi stahiki Ili watakapokuwa wakubwa wawe na hofu ya Mungu.

"Nguvu kubwa ya kumlea mtoto  ikitumika vizuri kuna matunda mazuri akiwa na utuuzima hivyo tujitahidi kuelekeza nguvu kwa watoto wetu," amesema.

Mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Wilaya ya Kibaha Mjini (UWT), Elina Mgonja amewataka wanawake mkoani humo kutiwafumbia macho baadhi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya ukatili kwa wananawake na watoto ili kujenga jamii yenye usawa.

Amesema kuwa Serikali inavyoendelea kupiga vita vitendo hivyo jamii inapaswa kushiriki kwa vitendo Ili kufikia mafanikio.