Wanawake wengi Tanzania wana vitambi

Dar es Salaam. Licha ya jitihada zinazofanywa na wanawake waishio mjini ikiwamo jijini Dar es Salaam, ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inaonyesha idadi ya wanaoelemewa na uzito inaongezeka.

Ripoti hiyo ya utafiti wa Ufuatiliaji wa Kaya (NPS) ya mwaka 2020/21 inaonyesha asilimia 47 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wasio na mimba, wana uzito uliopitiliza likiwa ni ongezeko la asilimia 8.2 kutoka mwaka 2014/15.

Ripoti hiyo iliyotumia kipimo cha ulingano wa uzito na urefu (BMI) inaonyesha vigezo vya mtu kuwa na uzito uliopitiliza ni kuwa na BMI kuanzia 25 na zaidi ya 30.

Takwimu hizo zinaonyesha katika kila wanawake wawili nchini, mmoja ana uzito uliopitiliza kutokana na kutumia vyakula vyenye mafuta mengi.

Kwa wanawake wanaoishi Dar es Salaam, ripoti imewaweka katika hali ya hatari zaidi kupata magonjwa ya shinikizo la damu, kisukari na saratani kutokana na uzito uliopitiliza kwani saba katika kila 10 wana hali hiyo.

“Wanawake wenye uzito uliopitiliza mwaka 2014/15 jijini Dar es Salaam walikuwa asilimia 52.7 lakini wameongezeka hadi asilimia 64.5 mwaka 2020/21,” inasema ripoti hiyo.

Asilimia 40.3 ya wanawake wanaoishi vijijini, ripoti inasema wana uzito uliopitiliza wakilinganishwa na asilimia 60.5 ya wanawake wa mjini.

Matokeo ya utafiti huu yanalingana na ule uliofanyika India mwaka 2013 na kuchapishwa katika Journal of Family Medicine and Primary Care ulioitwa ‘lishe na shughuli za kimwili miongoni mwa wanawake katika maeneo ya mjini na vijijini kusini mwa India’ ambao ulionyesha wanawake wa vijijini hawana uzito uliozidi kutokana na kufanya shughuli za kimwili mara tatu zaidi ya wanawake wa mjini.

Anastazia Mwelu (27), mkazi wa Sinza jijini Dar es Salaam mwenye uzito wa kilo 96 anasema ameshauriwa na daktari kuacha kula vyakula vyenye mafuta na wanga kwa wingi ili kupunguza uzito.

“Nilienda hospitali daktari alinishauri vyakula ambavyo sitakiwi kutumia kwa sasa zikiwamo chipsi ambazo nahisi zimenisababishia huu mwili. Pia, nimeambiwa niache kula vyakula vya wanga na nifanye mazoezi sana,” anasema Anastazia.

Katika hali ya mashaka na kutojiamini, Christina Joseph, mkazi wa Mbezi Beach jijini humo ana wasiwasi wa kuongezeka uzito kutokana na kukaa nyumbani muda mwingi baada ya kumaliza masomo yake ya chuo kikuu.

“Naona kabisa uzito wangu unaongezeka na nakuwa mvivu kwa sababu sina shughuli za kufanya baada ya kumaliza chuo, nikiamka asubuhi ni kula, kufanya shughuli za nyumbani na kulala. Naogopa kupima uzito, nahofu nitakuwa nimeongezeka uzito,” anasema Christina.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake katika Hospitali ya Salaaman, Abdul Mkeyenge anasema sababu ya wanawake kuwa na uzito mkubwa ni kutokula mlo kamili kama inavyoshauriwa.

Kwa kawaida, anasema kila binadamu anatakiwa kuwa na uwiano kati ya urefu na uzito wa mwili wake yaani BMI.

“Kwa kawaida, BMI inatakiwa kuanzia 18 mpaka 29.5 kwani zaidi ya 30 inamaanisha uzito uliopitiliza. Kuna sababu nyingi za mtu kuwa na uzito uliopitiliza lakini kubwa ni kutofuatilia mlo kamili,” anasema daktari huyo.”

Kitu cha msingi kuzingatia anasema ni kuepuka vyakula vyenye mafuta na sukari kwa wingi ambavyo wanawake wengi wanavipenda zaidi.

“Mji kama Dar es Salaam unakua kwa kasi na watu hawapangi ratiba ya kula vizuri, wanapenda kula vyakula vyenye mafuta na sukari na wanakunywa pombe kupitiliza,” anasema.

Vyakula vinavyoliwa mjini, daktari huyo anasema ni vya kusindika na huwekwa kwenye friji kwa muda mrefu hivyo kupoteza ubora.

Changamoto iliyopo, Dk Mkeyenge anasema ni mafuta kwenda kurundikana kwenye mishipa ya damu hali inayochochea uzito na kuzalisha shinikizo la damu kwa wanawake na wanaume.

Anasema kuzaa hakuna uhusiano wowote na uzito uliopitiliza kwani mtoto anapotengenezwa tumboni mwili huhitaji chakula kingi lakini wengi hawali mlo kamili ila wanajaza vyenye sukari na mafuta hivyo kujikuta wananenepa kupita kiasi baada ya kujifungua.

Daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake, Isaya Mhando anasema wanawake wengi huongezeka uzito baada ya kujifungua.

“Kuna sababu nyingi, mama anaweza kuongezeka uzito pindi kipato kinapoongezeka au kupungua kwa kazi alizonazo lakini wengi wanaingia kwenye tabia bwete kwa kutokufanya kazi, anatembelea gari akifika nyumbani anakaa tu kwenye kochi,” anasema.

Wanawake wengi, Dk Mhando anasema hawali vyakula vya asili na hawana elimu ya lishe bora.

“Kuna utafiti ulifanyika Kilimanjaro ulioonyesha kuna ongezeko la wanawake wenye vitambi huku kipato nacho kikiongezeka na maeneo yanayozalisha chakula ilionekana kuna watoto wana utapiamlo,” anasema Dk Mhando.

Utapiamlo, anasema huweza kujidhihirisha kwa kuwa na uzito kidogo au uliopindukia hivyo ni lazima watu wakafahamu wanapaswa kula vyakula gani na kufanya mazoezi na au kazi zinazoushughulisha mwili ikiwamo kulima.


Lishe bora

Ofisa Lishe Mtafiti Mwandamizi wa Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Walbart Mgeni anasema ni muhimu kila mtu kula mlo kamili ili kusaidia umeng’enywaji na ufyonzwaji wa chakula.

Kila mlo kamili, anasema unatakiwa kuwa na makundi yote matano ya vyakula vikiwamo vya nafaka, mizizi na matunda, mbogamboga, jamii za kunde na vyenye asili ya wanyama, mafuta na sukari bila kusahau kunywa maji safi.

“Tunachosisitiza mlo utokane na makundi hayo kwani unapokula zaidi sukari na mafuta unasababisha mwili kuongezeka. Wanawake wengi wanapenda vyakula hivyo kuliko wanaume,” anasema.

Mtaalamu wa Lishe wa Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila, Theresia Thomas anasema mlo kamili unatakiwa kuwa na mchanganyiko wa mbogamboga na matunda ambavyo huongeza kinga za mwili.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Saratani wa Hospitali ya Aga Khan, Dk Harrison Chuwa anasema ulaji usiofaa husababisha saratani ya mfumo wa chakula.

Dk Chuwa anasema miaka ya hivi karibuni wanapokea wagonjwa wengi wa saratani ikilinganishwa na miaka ya nyuma kutokana na mfumo mbaya wa maisha.

“Saratani hizi nyingi zimetokana na kula vyakula vya mafuta, kunywa pombe kali na kutofanya mazoezi,” anasema Dk Chuwa.