Wanne familia moja wafariki ajalini Morogoro

Muktasari:

Watu wanne wamefariki dunia kufuatia ajali ya lori na gari dogo aina ya Toyota Spacio katika eneo la Kwambe Dumila wilayani Kilosa mkoani Morogoro na kusababisha barabara kufungwa kwa saa kadhaa.

  

Morogoro. Watu wanne wamefariki dunia kufuatia ajali ya lori na gari dogo aina ya Toyota Spacio katika eneo la Kwambe Dumila wilayani Kilosa mkoani Morogoro na kusababisha barabara kufungwa kwa saa kadhaa.

Akizungumza na Mwananchi Digital kwa simu leo Januari 14 Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Majid Mwanga amesema gari hilo ndogo lilikuwa na watu sita akiwemo dereva ambaye ni mtumishi wa Serikali.

Mwanga amesema kwa sasa wanaendelea kufanya mawasiliano kujua ni mtumishi wa idara gani.

Aidha amesema imetambulika kuwa waliokuwemo ndani ya gari hiyo woye ni familia moja, ambapo aliwataka madereva kuendelea kuwa makini wanapokuwa barabarani hasa kwa kipindi hiki cha Mvua.

Mganga Mfawidhi wa hospitali ya Mtakatifu Joseph Dumila, Manyele Kapongo amesema wamepokea miili ya watu hao (marehemu) na majeruhi wawili.

Kapongo amesema kwa sasa wanaendelea na matibabu ya majeruhi hao wawili ambao ni mama na mtoto.

Aidha mashuhuda wa ajali hiyo wanasema kuwa magari hayo yaligongana uso kwa uso na ambapo gari ndogo imeharibika vibaya.

Shuhuda Julias Michael mkazi wa Dumila akizungumzia ajali hiyo amesema chanzo cha ajali hiyo ni kuendesha mwendokasi wa dereva wa gari ndogo kwa kushindwa kukwepa.