Wanne wakamatwa tena baada ya kufutiwa kesi, wakili azua tafrani
Muktasari:
- Washtakiwa hao ambao wote ni wafanyabiashara walikuwa wanakabikiwa na mashtaka 16 yakiwemo yakughushi stika za dawa zilizokwisha muda wake wa matumizi.
Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewafutia kesi wafanyabiashara wanne waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka 16 yakiwemo ya kula njama na kughushi stika za dawa zilizokwisha muda wake, kwa kuziongezea muda wa matumizi, baada ya kesi hiyo kushindwa kuendelea kwa muda mrefu.
Kesi hiyo iliyokuwa katika hatua ya usikilizwaji wa shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, imefutwa baada ya upande wa utetezi kuwasilisha ombi mahakamani hapo la kuifuta kesi hiyo kutokana na kutoendelea mara kwa mara.
Hata hivyo muda mfupi baada ya kuachiwa huru, washtakiwa hao walikamatwa tena na kuzua tafrani mahakamani hapo baina ya wakili wa utetezi dhidi ya askari Polisi walikuwa wanataka kuwakamata washtakiwa hao.
Washtakiwa hao walikuwa wanakabikiwa na kesi ya jinai namba 99 ya mwaka 2019 yenye mashtaka 16, ambapo mashtaka 15 kati ya hayo; ni ya kughushi stika za dawa zilizoisha muda wake na shtaka moja ni la kula njama ya kutenda makosa ya kughushi.
Waliofutiwa kesi hiyo ni Khalid Somoe (54) mkazi wa Keko Mwanga; Raphael Lyimo (40), mkazi wa Kimara Bonyokwa; Betty Mwakikusye(41) mkazi wa Chanika Msumbiji na Abdiel Mshana(57) mkazi wa Msasani Ubalozini, wote ni wakiwa ni wafanyabiashara.
Uamuzi wa kuifutia kesi hiyo umetolewa leo Mei 23, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Romuli Mbuya wakati shauri hilo lilipoitwa kwa ajili kuanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka.
Hakimu Mbuya ameifuta kesi hiyo chini ya kifungu namba 225(5) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Hii ni baada ya Wakili wa Serikali, Faraji Ngukah kueieleza Mahakama hiyo kuwa shahidi upande wa mashaka yupo mbele ya mahakama hiyo, japo mtunza vielelezo wa kesi hiyo amepata dharura na hivyo kushindwa kufika mahakamani na kwamba kutokana na hayo wanaomba kesi hiyo iendelee kesho.
"Mheshimiwa hakimu, kesi hii imeitwa kwa ajili ya upande wa mashtaka kuanza kutoa ushahidi na tayari tunaye shahidi mmoja hapa mahakamani, lakini mtunza vielelezo katika kesi hajafika mahakamani hapa kwa sababu amepata dharura, hivyo tunaiomba mahakama yako iahirishe kesi hii hadi kesho ili tuweze kuendelea na ushahadi," amedai Ngukah.
Baada ya maelezo hayo, upande wa utetezi ukiongzwa na Wakili Agath Fabian akishirikiana na Baraka Mkama, aliomba Mahakama hiyo kuifuta kesi hiyo chini ya kifungu namba 222 cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA).
Hata hivyo ombi hili lilipingwa na wakili Ngukah kwa madai kuwa kifungu hicho kinatumika pale ambapo mlalamikaji hayupo mahakamani wakati upande wa mashtaka walikuwepo mahakamani hapo.
"Mheshimiwa hakimu kifungu alichotumia wakili mwenzangu kinatumika tu pale ambapo mlalamikaji hayupo mahakamani...lakini sisi tupo hapa mahakamani, hivyo naomba utupilie mbali ombi hili," amedai Ngukah.
Hakimu Mbuya baada ya kusikiliza maelezo ya mawakili wa pande zote, alikubaliana na ombi la upande wa utetezi na kuifuta kesi hiyo kwa maelezo kuwa kesi hiyo imekuwa haiendelei na usikilizwaji kwa muda mrefu.
Wakamatwa tena
Muda mfupi baada ya washtakiwa hao kufutiwa kesi na kuachiwa huru, walikamatwa tena na Polisi waliokuwepo katika viunga vya Mahakama.
Baada ya washtakiwa hao kukamatwa, mmoja wa wakili wa washtakiwa hao, Baraka Mkama alipinga kitendo cha wateja wake kukamatwa mahakamani hapo, akishinikiza washtakiwa hao waachiwe na hivyo kuzuia mvutano mkali.
Mvutano huo ulizua taharuki hadi katika lango kuu la kuingilia mahakamani hapo, ambapo askari waliokuwepo mahakamani hapo walimkamata wakili huyo kwa kile walichodai kuwa anawazuia wasifanye kazi yao.
Baada ya kuwepo kwa mvutano mkali baina ya washtakiwa na wakili Mkama, Askari Polisi Mbaraka Liyongo na Ibrahim Shabani walienda kufunga geti na wakiwa katika harakati hizo, wakili huyo alifungua geti la mahabusu waliyokuwa wakishikiliwa, kisha kumfungua mmoja wa wateja wake.
Kutokana na hali hiyo askari Polisi ilibidi watumie nguvu za kuwadhibiti washtakiwa hao pamoja na wakili wao Mkama.
Askari hao baada ya kufanikiwa kumdhibiti wakili Mkama na mshtakiwa Somoe, waliwaweka chini ya ulinzi na kuwapelea chumba cha mahabusu kilichopo mahakamani hapo wakisubiri taratibu nyingine za kisheria, huku mshtakiwa mmoja Betty akifanikiwa kutoka nje ya geti kuu na kukimbia.
Hata hivyo muda mfupi baadae gari la Polisi aina ya Landcruse lilifika mahakamani hapo na kumchukua wakili huyo wa utetezi Mkama pamoja na mshtakiwa Somoe na kuwapakiza katika gari hiyo na kisha kuwapeleka kituo Kikuu cha Polisi Central.
Hati ya mashtaka
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa yao kati ya Machi Mosi na Machi 31, 2019 katika maduka mbalimbali ya dawa yalipo katika mkoa wa Dar es Salaam.
Katika shtaka la kula njama za kutenda kosa la kughushi, washtakiwa kwa pamoja wanadaiwa kati ya Machi Mosi 2019 na Machi 31, 2019 maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, walikula njama ya kughushi.
Miongoni mwa shtaka moja la kughushi kati ya mashtaka 15 ya kughushi yanayowakabili washtakiwa hao, kwa pamoja wanadaiwa Machi 18, 2019 katika mtaa wa Amani na Simba uliopo Kariakoo Wilaya ya Ilala, kwa nia ovu, walighushi stika za mbalimbali za dawa kwa lengo la kuonyesha kuwa stika hizo ni halisi na zimetolewa na Kiwanda cha Keko Pharmaceutical Industries (1997) wakati wakijua kuwa ni uongo.
Hata hivyo Washtakiwa walikuwa nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana.